Watumishi Moshi wafundwa madhara ya dhuluma

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, akizungumza na watumishi wa manispaa hiyo.

Muktasari:

Watumishi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameagizwa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na kuepuka dhuluma kwa wanaowaongoza na kuwasimamia.

Moshi. Watumishi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameagizwa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na kuepuka dhuluma kwa wanaowaongoza na kuwasimamia.

Mbali na hilo, wametakiwa kuepuka kuzungumza mambo yaliyo nje ya mipaka yao, hali inayosababisha mpasuko katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unaotarajia kufanyika baadaye mwaka huu, na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema hayo leo Machi 18, 2024 alipofungua kikao kazi cha watumishi viongozi katika ngazi ya kata na mitaa wa halmashauri hiyo, kilichofanyika ukumbi wa Shule ya Sekondari Moshi.

Nasombe amesema watumishi wote waliopewa dhamana ya uongozi, wanapaswa kusimama kwenye haki na kutanguliza mbele masilahi ya Taifa ili kuwezesha dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo kufikiwa kikamilifu.

"Tusiache kumtanguliza Mungu kwenye kila tunachofanya, niwakumbushe watumishi wenzangu, hakuna kitu kibaya kama dhulma, dhulma ni mbaya, wakati mwingine unaweza kuona unafanya mambo yako hufanikiwi, kumbe kuna nafsi zinalia kwa ajili yako,” amesema.

Ameongeza: "Unashangaa kila unachofanya hakiendi mbele, kumbe unawadhulumu watu wengi na machozi ya watu wasiokuwa na hatia lazima uyalipie, usipolipa wewe watalipa kizazi chako."

“Kwa hiyo tujiepushe katika dhulma, kwenye haki tusimamie haki, lakini ukishindwa kabisa kuzungumza mazuri basi ni vizuri ukakaa kimya, kwani itakapotokea mtumishi mwenye dhamana ukazungumza vitu ambavyo si salama, vitasambaa zaidi kuliko akizungumza muuza mbogamboga, kwa sababu wanaamini wakizungumza watumishi wa umma siku zote wanazungumza ukweli," amesema.

Amesema kama watumishi wa umma ni lazima wajue uwajibikaji wao uko katika maeneo gani, wakati gani wanatakiwa kufanya nini na kusema nini.

"Watumishi wenzangu, tunaenda kwenye maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Vibweka hapa katikati vitakuwa vingi sana, usishawishike kuzungumza kitu ambacho hukifahamu,” amesema.

Judith Mahende, Mkuu Divisheni ya Utumishi na Utawala wa Manispaa ya Moshi, amewataka watumishi kutumia madaraka yao vizuri na kuepuka kutumia nafasi zao kuwakandamiza wengine.

"Katika msingi wa maadili, uadilifu ni sehemu; watumishi wa umma tunapaswa kutumia madaraka tuliyokabidhiwa kwa kuzingatia mipaka ya madaraka yetu na hatupaswi kutumia madaraka haya kwa manufaa binafsi, kwa kuwakandamiza wengine kwani tunapokiuka tunakuwa tumeenda nje ya uadilifu na hatujafuata misingi ya maadili," amesema.

Katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zilitolewa zikiwamo za maadili ya utumishi wa umma, taratibu za ununuzi, sheria na taratibu za mapato.