Watumishi: VAT iondolewe kwenye nyumba

Muktasari:

Muuguzi katika hospitali ya umma, Zilpha Kalonzo alisema Serikali inapaswa iwaangalie kwa jicho la tatu kwani mishahara yao ni duni

Dar es Salaam. Watumishi wa umma mkoani Morogoro wameiomba Serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika uuzaji wa nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na Kampuni ya Nyumba za Watumishi (WHC).

Walisema juzi kuwa kuwapo kwa kodi katika uuzaji wa nyumba hizo kunaondoa uhalisi wa neno nyumba za gharama nafuu kwa watumishi wa umma.

“Bei ya nyumba hizi kabla ya VAT zinakuwa zinavutia na kuwa na dalili ya uwezekano wa kuzinunua, lakini inapokuja kodi tarakimu za bei zinabadilika na kuwa za kutisha, hata hamu ya kununua nyumba hizo inapotea,” alisema Daud Mganga.

Muuguzi katika hospitali ya umma, Zilpha Kalonzo alisema Serikali inapaswa iwaangalie kwa jicho la tatu kwani mishahara yao ni duni na hawana namna ya kupata fedha za ziada zaidi ya kutegemea malipo yao ya uzeeni.

“Sisi watumishi wa uuma tunategemea mishahara, kiinua mgongo na mikopo ya benki. Namuomba Rais John Magufuli aaimuru TRA iondoe kodi katika nyumba za gharama nafuu,” alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa WHC, Dk Fred Msemwa alisema  mradi wa ujenzi wa nyumba 40 kati ya 70 za awamu ya kwanza umekamilika.

Dk Msemwa alisema makali ya kodi yanaathiri lengo zima la kuwapatia watumishi wa umma makazi bora na ya gharama nafuu.

“Athari ya kodi ya ongezeko la thamani VAT ni kubwa sana kwa wateja wetu. Wengi inawakimbiza au kuwabagua na kujikuta wanakimbilia katika makazi yasiyojengwa kwa mpango na maeneo yasiyopimwa,”alisema.