Watumishi wa halmashauri kizimbani kwa madai ya kujaribu kuua

Muktasari:

Watu watatu wakiwemo watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo wakituhumiwa kwa kosa la kujaribu kumuua Ofisa Utumishi wa halmashauri hiyo, Mussa Abdallah (38) mkazi wa Mtaa wa Mwayunge Kata ya Igunga mjini.

Tabora. Watu watatu wakiwemo watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo wakituhumiwa kwa kosa la kujaribu kumuua Ofisa Utumishi wa halmashauri hiyo, Mussa Abdallah (38) mkazi wa Mtaa wa Mwayunge Kata ya Igunga mjini.

Watu hao waliofikishwa jana Aprili 13, 2023 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Edda Kahindi ni aliyekuwa Kaimu Ofisa Ardhi wa halmashauri hiyo ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Jahulula Edward Jahulula (41).

Mwingine ni Mhandisi wa halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Emmanuel Ikandiro (48)  na Mkulima wa Kata ya Mbutu wilayani humo, Masanja Bukwimba (43).

Mwendesha mashitaka wa Polisi, Ellymajid Kweyamba ameiambia Mahakama kuwa washitakiwa  wote watatu wanakabiliwa na shitaka moja la kujaribu kuua.

Amesema usiku wa Machi 10, 2023 katika Mtaa wa Mwayunge Kata ya Igunga mjini  washitakiwa wakiwa na nia ovu walijaribu kumuua Ofisa huyo kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni wakati akiwa amepumzika nyumbani kwake baada ya kutoka kwenye kikao cha baraza la madiwani.

Hata hivyo baada ya kusomewa shitaka hilo ,washtakiwa wote watatu hawakutakiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprilii 25, 2023 itakapotajwa tena na watuhumiwa wote wako nje kwa dhamana ya Sh3 milioni kwa kila mmoja.