Watumishi wanne afya wafukuzwa kazi Arusha

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Charles Rashid Mkombachepa

Muktasari:

  • Wahudumu wanne wafukuzwa kazi, watatu wasimamishwa kwa mwaka mmoja, madaktari bingwa wanne wameshtakiwa kwenye Baraza la Madaktari kwa makosa mbalimbali.

Arusha. Wahudumu wanne katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, wamefukuzwa kazi baada ya kubainika kufanya makosa ya kitaaluma na kinidhamu, ikiwemo matumizi ya lugha mbaya kwa wagonjwa.

Mbali na hao, wengine watatu wamesimamishwa kazi kwa mwaka mmoja kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kuomba rushwa na kufanya mzaha kazini.

Pia madaktari bingwa wanne mashauri yao yanaendelea katika Baraza la Madaktari na kamati za nidhamu kwa tuhuma za makosa ya kitaaluma na kutotoa huduma stahiki kwa wagonjwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Charles Mkombachepa amesema hayo jana kwenye mdahalo wa kutathmini mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, ulioandaliwa na waandishi wa habari mkoani Arusha na kufanyika katika viwanja vya Stendi Kuu ya mabasi.

Amesema adhabu hizo zimetolewa kwa kipindi cha miaka miwili 2021/2022 na 2022/2023 kama funzo kwa wahudumu wa afya, kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao wa kufuata maadili ya taaluma zao, ikiwemo kuwahudumia wananchi kwa upendo na unyenyekevu.

Amesema wawili waliofukuzwa kazi walikuwa wanahudumu kitengo cha maabara walibainika kutoa majibu yasiyo sahihi kwa wagonjwa na mmoja ni mtaalamu wa tiba ya viungo aliyetiwa hatiani kwa kosa la ulevi kazini. Mwingine alikuwa mhasibu aliyekutwa na makosa ya wizi.

Amesema madaktari wawili walisimamishwa kazi kwa kuomba rushwa na lugha zisizo na staha, huku muuguzi mmoja akibainika kufanya mzaha kazini.

Dk Charles amesema madaktari bingwa wawili mashauri yao yako Baraza la Madaktari kwa makosa ya kitaaluma na wengine wawili wako katika kamati za nidhamu kwa makosa ya kutotoa huduma stahiki kwa wagonjwa.

“Hatuwezi kumvumilia wala kumuonea huruma mtumishi mzembe ambaye anapaka tope taswira ya Serikali kwa wananchi wetu, na hii ikawe funzo kwa wengine mkoa mzima kwani tutaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaobainika kukengeuka,” amesema.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetoa zaidi ya Sh33.17 bilioni kwa ajili ya huduma za afya mkoani Arusha, ikiwemo kuboresha miundombinu.

Amesema fedha hizo zimejenga zahanati 44, vituo vya afya 21, na wodi za kujifungua wajawazito katika vituo 17.

Katika mdahalo huo, mkazi wa Arusha, Patrick Mtemi amesema baadhi ya watumishi wa afya wamekuwa kero na wakatili kwa wagonjwa kutokana na majibu yao mabaya, lakini pia huduma zinazotangazwa kuwa bure zimekuwa dili kwa wahudumu.

“Serikali inasema huduma ni bure kwa mtoto chini ya miaka mitano kuanzia vipimo hadi dawa lakini pia vifaa vya kujifungua, lakini uhalisia si kweli,” amesema.

Korumba Moshi, ambaye ni mwandishi wa habari amesema lengo la mdahalo huo ni kuwapa wananchi jukwaa la kutathmini utekelezaji wa shughuli za Serikali.