Wawili matatani Moshi kwa wizi betri kwenye minara ya simu

Muktasari:

  • Washtakiwa hao ambao ni Fadhili Pascal pamoja na Gelard Gelard wakazi wa Mianzini mkoani Arusha, wamefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Salome Mshasha huku upande wa Jamuhuri ukiwakilishwa na Mwendesha mashitaka wa serikali Sabitina Mcharo

Moshi. Watu wawili wamefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, mkoani Kilimanjaro wakishtakiwa kwa kosa la wizi wa betri 12 za minara ya simu.

Watu hao ni Fadhili Pascal na Gelard Gelard ambao ni wakazi wa Mianzini mkoani Arusha na wamefikishwa Mahakamani mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Salome Mshasha huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Sabitina Mcharo.

Akisoma maelezo ya kosa, Sabitina amesema kuwa, Novemba 23, 2022 katika maeneo ya Kibosho wilaya ya Moshi, washitakiwa hao waliiba betri 12 za  minara ya simu ya kampuni ya Vodacom.

Washitakiwa hao walikana kosa hilo ambapo Hakimu Mshasha ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 8, 2022 ambapo itakuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 2 ya mwaka 2023, Mshitakiwa Gerald aliachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi vigezo huku Fadhili akienda mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Akizungumza nje ya mahakama msimamizi wa masuala ya ulinzi wa mkoa wa Kilimanjaro kutoka kampuni ya ulinzi  inayohusika na ulinzi wa minara hiyo (Intelligence Securico Limited), Ambrose Sangawe amesema wizi huo ulifanyika katika minara ya simu iliyopo eneo la  Hospitali ya Kibosho na kwamba ulisababisha athari mbalimbali ikiwemo kuathiri mawasiliano na kipato kwa wananchi.

Amesema washtakiwa hao ni mafundi ambao wamekua wakifanya shughuli za kiufundi kwenye minara ya mawasiliano ambao wanajua umuhimu, thamani, uwezo na soko la betri hizo.

"Wizi huu wa betri kwenye minara ya mawasiliano umeleta athari kubwa  kwa wateja wetu  na wananchi ambao ni  watumiaji wa mawasiliano katika shuhuli mbalimbali, tunalishukuru jeshi la polisi ambao wameweza kutusaidia na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wawili ambao wamekua wakihusika kwa wizi wa betri hizo," amesema.