Wawili mbaroni tuhuma za kujipatia fedha kwa njia zisizo halali

Kamanda wa Jeshi la Polisi Manyara, RPC George Katabazi akizungumza na vyombo vya habariĀ leo Mei 18, 2023. Picha na Mohamed HamadĀ 

What you need to know:

  • Watuhumiwa hao ni Mohamed Saidi (Van dume) na Diana Loy wakazi wa Dar es Salaam ambao walikutwa katika nyumba ya kulala wageni mjini Babati

Babati. Jeshi la Polisi Mkoani Manyara lashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na Sh20 milioni ambazo zinasadikiwa kupatikana katika njia zisizo halali ikiwemo wizi na uvunjaji wa nyumba pamoja na maduka katika mkoa wa manyara na simu 27.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Manyara RPC George Katabazi leo Alhamisi Mei 18, 2023 amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed Saidi (Van dume) na Diana Loy wakazi wa Dar es Salaam walikamatwa wakiwa katika nyumba ya kulala wageni mjini hapa.

"Fedha hizo zinadhaniwa kupatikana kwa njia isiyo ya halali ikiwemo wizi wa uvunjaji wa nyumba na maduka katika mkoa wa Manyara. Vile vile hizi simu 27, zinadhania pia kupatikana katika matukio ya wizi pamoja na uvunjaji," Amesema Kamanda huyo.

Ameongeza: "Kwa hiyo hapa kuna mali mbalimbali kuna vitambulisho lakini pia kuna vifaa vya simu vyote hivi vimepatikana kwa njia hiyo isiyo halali kupitia matukio ambayo nimeyataja hapa."

Katika hatua hiyo RPC Katabazi ametoa wito kwa wananchi kufika Babati kutambua mali hizo ili kujua kama ni zao

"Sio hawa tu kuna mtandao wa wengine na wao wamekimbilia maeneo ya jirani ya mkoa wetu wa Manyara, Arusha Singida na Dodoma...tunaendelea kuufuatilia tukiwa na lengo la kuvunja na kuhakikisha kuwa uhalifu wa uvunjaji na wizi katika mkoa wetu wa Manyara tunautokomeza," amefafanua.

Amesema mpaka sasa kuna mafanikio makubwa ya kuwakamata watu wenye kufanya uharifu wa aina hiyo, na kwamba polisi inaendelea kuwasaka wengine akidai ni jambo la wakati tu ukifika nao watakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.