Wawili wafa kwa ajali msafara wa Dk Biteko

Mashuhuda wakiangalia gari lililopata ajali kwenye msafara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na kusababisha vifo vya watu wawili, mpigapicha wa Tanga Televisheni, Ally Nassor na Dereva wa gari la Tanga Uwasa, Said Omar Alawi na kujeruhi watu wengine wawili, wilayani Korogwe leo Januari 26, 2024.

Muktasari:

  • Ajali imetokea leo Januari 26, 2024 katika Kijiji cha Mamboleo barabara ya Tanga-Segera wakati msafara wa Waziri Mkuu ukitoka jijini Tanga kwenda kituo cha kufua umeme cha Hale wilayani Korogwe.

Tanga. Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni Tanga (TaTV), Ally Hassan Haroun na dereva wa gari la Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa), Said Omar Alawi wamefariki dunia katika ajali iliyotokea kwenye msafara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Ajali hiyo imetokea leo Januari 26, 2024 katika Kijiji cha Mamboleo barabara kuu ya Tanga-Segera wakati msafara huo ukitoka jijini Tanga kwenda Kituo cha kufua umeme cha Hale wilayani Korogwe.

Katika ajali hiyo, watu wanne walijeruhiwa na kupelewa Hospitali ya Teule ya wilayani Muheza na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo.

Waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga wakiwa katika majonzi nje ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, Bombo baada ya kupewa taarifa kuwa mwenzao amefariki dunia baada ya ajali iliyotokea kwenye msafara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko. Katika ajali hiyo pia alifariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa.

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Bombo, Frank Shega amewataja majeruhi hao kuwa ni Frank Godfrey, Ali Hassan Haroun, Salum Hamis Ngumbi na Said Omari ambaye ni dereva wa gari hilo.

"Tuewapokea majeruhi Said Omar, Frank Godfrey na Salum Ngumbi lakini mwandishi wa habari, Ally alifia njiani na Said ambaye ni dereva amekufa saa 5:30wakati akiendelea na matibabu ilikuwa," amesema Dk Shega.

Mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa Tanga Televisheni, Ally Haruna aliyefariki kwenye ajali katika msafara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko yakiendelea katika makaburi ya Sharif Haidar leo Januari 26, 2024

Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Habari wa Uwasa Tanga, Devotha Mayala amesema dereva aliyekufa katika ajali hiyo alihamishiwa mkoani Tanga hivi karibuni akitokea Wizara ya Maji na alikuwa anafanya kazi katika mradi wa maji wa Serikali katika miji 28

"Said ni mgeni hapa Tanga, ameletwa hapa kupitia mradi wa miji 28 lakini Mungu amemchukua," amesema Devotha.

Awali, taarifa ya ajali hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Abdurahman Rajabu katika mkutano wa hadhara wa Naibu Waziri Mkuu uliofanyika Kijiji cha Kilapula Wilaya ya Muheza kabla ya taarifa za vifo kufahamika.

"Tunashukuru Naibu Waziri Mkuu ziara yako ilikuwa ya mafanikio umetusaidia sana mkoa wetu, japo asubuhi imetokea ajali iliyojeruhi,” alisema Rajabu.

Akizungumzia ajali hiyo, Dk Biteko aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Tanga na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhakikisha majeruhi wanapatiwa matibabu kwa hali na mali.

"Niwape pole majeruhi wa ajali hiyo, nakuagiza Waziri wa Afya na uongozi wa mkoa shughulikieni matibabu yao," alisema Dk Biteko.

Baada ya Biteko kuagwa katika Uwanja wa Ndege wa Tanga, waandishi wa habari walienda Hospitali ya Bombo na kufahamishwa kuwa mwanahabari mwenzao na dereva wamefariki dunia.

Biteko alikuwa Tanga kwa ziara ya siku tatu ambapo alitembelea mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, Kituo cha kupimia mafuta yanayopingia katika Bandari ya Tanga, ghala la kuhifadhi mafuta la GBP na miradi ya kupeleka umeme vijijini REA.