Wawili wafariki magari yakigongana na kuwaka moto Mbozi

Muktasari:
- Watu wawili wamefariki na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili likiwamo lililobeba mafuta na kuwaka moto katika ajali iliyotokea maeneo ya Old Vwawa wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe.
Songwe. Watu wawili wamefariki na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili likiwamo lililobeba mafuta na kuwaka moto katika ajali iliyotokea maeneo ya Old Vwawa wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe.
Ajali hiyo imetokea jana Machi 7, 2022 majira ya saa 8.00 mchana ambapo wakazi wa Mji wa Vwawa walianza kuona moshi mkubwa mweusi kwa mbali ukipanda angani ambapo baadaye walielezwa ni wa kuungua magari mawili eneo la Old Vwawa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, Rashid Ngonyani amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema lori lililobeba mafuta lilipata hitilafu baada ya gari dogo aina ya Nissan kuligonga lori hilo na yote yakawaka moto.
Amesema kati ya watu waliokufa ni mtoto anayekadiriwa kuwa na mwaka mmoja ambaye mwili wake uligundulika ndani ya gari dogo na mwili wa mtu mzima uliokutwa kwenye lori.
Amesema watu watatu waliokuwa kwenye gari dogo waliokolewa na kupelekwa haraka hospitali ya Vwawa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba alifika eneo la tukio na kushiriki kazi ya uokoaji na kuondoa magari barabarani ili kuruhusu nagari mengine kupita.
RC Mgumba amesema tatizo barabara hiyo ni nyembamba mno na hivyo kusababisha foleni ndefu na ajali.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudiwa foleni kubwa ya magari yanayoelekea mji wa Tunduma katika mpaka wa Tanzania na Zambia.