Wawili wakamatwa na kilo 12 za bangi Singida

Muktasari:

  • Jeshi la polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kukutwa na dawa ya kulevya aina ya bangi misokoto 2,619 yenye uzito wa kilogramu 12.

  

Singida. Jeshi la polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kukutwa na dawa ya kulevya aina ya bangi misokoto 2,619 yenye uzito wa kilogramu 12.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakati wa msako uliofanyika kati ya Aprili Mosi hadi 16, 2022.

Amewataja watuhumiwa hao ni pamoja na mwanamke mmoja (29), ambaye alikamatwa na misokoto 1,948 sawa na kilogramu 10.

“Mtuhumiwa huyo alitumia mbinu ya kuweka madawa hayo katika mfuko wa sandalusi na kuificha kwenye banda la kufugia kuku. Lengo ni kusambaza bangi hiyo kwa wateja wake ambao ni watumiaji wa madawa hayo kwa kificho,”amesema.

Kamanda Stella amemtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni mkazi wa eneo ya kata ya Kindai manispaa ya Singida

“Tumemkamata mtuhumiwa wa pili Aprili 12,2022 saa 8.30 mchana akiwa na bangi misokoto 761 yenye uzito wa kilogramu 02. Bangi hiyo aliihifadhi kwenye mfuko wa sandarusi na kuiweka chini ya kitanda chake,”amesema.

Amesema kwa sasa majina ya watuhumiwa hao, hawezi kuyataja kwasababu upelelezi bado unaendelea ili kubaini mtandao wao.

Aidha, Kamanda Stella amesema Aprili 9, 2022 Saa 3.00 asubuhi katika maeneo ya Kijiji cha Ulyiampiti Wilaya ya Ikungi mkoni Singida, walimkamata Emmanuel Juma (29) kwa tuhuma ya kumiliki mafuta ya dizeli lita 300 yanayodhaniwa kuwa ni ya wizi.

Kamanda huyo amesema dizeli hiyo iliwekwa kwenye madumu 18 yenye lita 20 kila moja.

Amesema upelelezi bado unaendelea kuhusu upatikanaji wa mafuta hayo ambayo mtuhumiwa anayauza kwa bei poa.

Katika hatua nyingine, Kamanda Stella amesema kuelekea Sikukuu ya Pasaka, jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha mkoa unakuwa salama kwa kufanya misako ya doria za miguu, magari, pikipiki na doria za mbwa.