Wazanzibari wakumbushwa kumuenzi Karume

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla

Muktasari:

  • Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amewataka wananchi visiwani humo kumwenzi mwasisi wa nchi hiyo marehemu Abeid Karume kwa kuchapa kazi.

Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati Wazanzibari wakiwa kwenye kumbukizi ya kifo cha mwasisi wa nchi hiyo, hayati Abeid Aman Karume, ni vyema kuishi katika misingi ya uchapakazi ili kufuatya alama alizoacha kiongozi huyo.

Ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2023 wakati wa kongamano la tano la maadhimisho ya kumbukizi ya kifo cha Karume lililoandaliwa na kufanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume, Zanzibar.

Abdulla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo ametaka kumuenzi Karume katika misingi ya uwazi, uadilifu, ushirikishwaji, upendo na umoja ili kuishi na kuendeleza yaliyoasisiwa na kiongozi huyo.

"Kila mmoja kwa nafasi yake tumuenzi Karume katika misingi ya uchapakazi tukilenga kuacha alama katika maisha yetu. Mzee Karume hayupo leo ni miaka 51 lakini bado alama zake zinaonekana na zitaendelea kuishi," alisema Abdulla.

Hata hivyo amewataka wanaondika historia ya kiongozi huyo kuandika ukweli kama ilivyotokea ili kuweka uwazi na kusaidia vizazi vijavyo kutambua taifa lilipotoka, lilipo na mwelekeo wake wa baadaye.

Amesema serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa kuimarisha sekta za kijamii, kisiasa na kiuchumi na kuendelea kuweka mazingira bora ya amani na utulivu yanayowezesha taifa kukua kiuchumi.

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho, Stephen Wasira amesema ipo haja kuandika historia ya marehemu Karume kama ilivyotokea kabla ya mapinduzi.

"Lazima tumkumbuke marehemu Karume kwa historia ya kazi yake nzima kama mpigania uhuru kama walivyo wapigania huru wengine wa wanaotajwa Afrika," amesema Wasira.

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Professa Shadrack Mwakalila alisema lengo la kuendesha makongamano hayo ni kujadili na kuendeleza fikra za kiongozi huyo katika nyanja mbalimbali za kukuza elimu na ustawi wa jamii.

Amesema Chuo hicho kilianza na wanafunzi 22 lakini kwa sasa kina wanafunzi zaidi ya 2500 na hiyo ni ishara kwamba wazazi wamebadilika na kuona umuhimu wa kuwapatia watoto wao elimu.

"Hapa tunajikumbusha misingi mikubwa aliyoijega Mzee Karume ni sehemu ya historia muhimu inayotakiwa kufundishwa kwa vijana," amesema.