Wazazi wa wanafunzi bora wazungumza
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa, Dar es Salaam, wasichana wamefanya vizuri zaidi kwa kunyakua nafasi saba kati ya kumi bora kitaifa.
Muktasari:
- Katika matokeo hayo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa, Dar es Salaam, wasichana wamefanya vizuri zaidi kwa kunyakua nafasi saba kati ya kumi bora kitaifa.
Dar es Salaam. Wazazi wa wanafunzi kumi bora katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika mwaka jana, wameeleza kufurahishwa na matokeo hayo, huku mwingine akisema alitabiri mapema ushindi huo.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa, Dar es Salaam, wasichana wamefanya vizuri zaidi kwa kunyakua nafasi saba kati ya kumi bora kitaifa.
Siri ya mafanikio ya Robina
Baba mzazi wa mwanafunzi, Robina Nicholaus aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, Benard Nicholaus alisema binti yake alianza kuonyesha dalili ya mafanikio ya kitaaluma tangu alipokuwa darasa la kwanza.
Mzazi huyo ambaye ni Ofisa Mawasiliano wa Wizara Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, alisema binti yake alipomaliza mitihani alimhakikishia matokeo mazuri na kumwomba asiwe na wasiwasi.
Alisema maadili mema na jitihada binafsi za binti yake akiwa shuleni zimechangia sehemu kubwa ya matokeo aliyoyapata, pamoja na kurithi akili nzuri kutoka kwa wazazi, kwani wote wawili wana Shahada za Uzamili.
Nicholaus aliongeza kuwa tabia ya binti yake ya kukwepa kujichanganya na makundi yasiyofaa ya wasichana wenzake ndiyo inayomwezesha kupata muda wa kutosha kusoma na kumwomba Mungu.
“Huyu mtoto hatujawahi kutumia nguvu yoyote kumwonya kwa jambo lolote, yeye mwenye anajua kitu gani kinamfaa,” aliongeza.
Robina azungumza
Akizungumzia matokeo yake, Robina alisema kuwa amepata alama A nane na B mbili, jambo litakalomwezesha kutimiza ndoto ya mama yake ambaye alitaka kuwa daktari, lakini alishindwa kutokana na matatizo ya kiafya.
“Matokeo hayo yamenishangaza kwa sababu yanataka kufanana na aliyoyapata mama yangu. Yeye alipata A mbili na B nane,”alisema.
Alifafanua kuwa awali alitamani kuwa muuguzi, lakini baada ya kuona watu kama wanawadharau wauguzi akaona ni bora baadaye awe daktari ingawa hajafahamu atasomea udaktari gani.
Akisimulia anavyojisikia tangu alipopata taarifa kuwa ndiye mwanafunzi wa kwanza kitaifa, Robina alisema: “Nina furaha sana. Jana (juzi) nilichelewa kulala. Huwa nalala saa tano, lakini nililala saa saba usiku, hata asubuhi nimeamka mapema sana, sina usingizi.”
Kauli ya mama
Mama mzazi wa Robina, Pili Mogasa alisema tangu binti yake aliposikia matokeo hayo amekuwa mwenye furaha kuliko kawaida huku akishindwa kula vizuri.
“Jana nilikuwa nikimwangalia wakati akila. Alitumia muda mrefu zaidi. Siyo kawaida yake. Nilijua anatafakari matokeo hayo,” alisema Pili.
Naye Eliamani Mwamgigal ambaye ni bibi wa mwanafunzi huyo alisema anaamini mafanikio ya mjukuu wake yanatokana na tabia ya binti huyo, kumwogopa Mungu.
Alisema tangu akiwa kidato cha kwanza alikuwa akimwambia kwamba siri pekee ya mafanikio katika maisha ni kumwomba Mungu kila wakati.
“Siku zote tulikuwa tunaomba pamoja jioni. Ameendelea kufanya hivyo hadi sasa, ndiyo maana amefaulu,” alisema bibi yake.
Bibi huyo ambaye ni mkunga mstaafu aliongeza: “Nilikuwa namsimulia historia ya maisha yangu, nilikuwa wa kwanza katika masomo yote niliyowahi kusoma. Mungu ndiye aliyenisaidia.”
‘Wametimiza ndoto yangu’
Mzazi wa mwanafunzi Joyceline Marealle, aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa katika mtihani huo, Leonard Marealle, alisema matokeo hayo yametimiza ndoto yake ya kuhojiwa na waandishi wa habari.
Akizungumza nyumbani kwake Boko, Dar es Salaam jana, Marealle alisema kabla ya kuanza kwa mitihani hiyo mwaka jana aliwaambia binti zake (Joyceline na Eve), ambao ni pacha kuwa watafaulu kwa kiwango kikubwa kiasi cha waandishi wa habari kuwatafuta wazazi wao.
Alisema Joyceline ambaye amepata daraja la kwanza pointi saba, Eve pia ameibuka na daraja la kwanza akiwa na pointi 11. Walionyesha mapema dalili za kuibuka wanafunzi bora.
“Sijawahi kuona mabinti wanaosoma namna hii, wakitoka shuleni saa kumi na moja jioni, wanakula halafu wanakwenda kupumzika, saa tano wanakutana kusali, wanasali sana hawa,” alisema Marealle.
Mama mzazi wa wanafunzi hao, Caroline Munuo alisema kuwa kila siku mume wake alikuwa akitabiri kwamba matokeo ya kidato cha nne yatawakutanisha wazazi hao na wanahabari, lakini yeye alikuwa haamini.
“Alikuwa akisema kila siku, lakini mimi nilikuwa siamini hadi leo (jana) mlipokuja (waandishi) kwa ajili ya kutuhoji, ndiyo naamini sasa,” alisema Caroline.
Aliongeza kuwa katika kuthibitisha kwamba alikuwa anamaanisha jambo alilokuwa akisema, baba yao aliamua kuwapeleka binti zake shuleni mwenyewe kipindi chote cha kufanya mitihani.
“Niliamua wasiende na basi la shule. Niliwapeleka mwenyewe. Kwa kweli nilikuwa nafanya nao mitihani, maana wakitoka nilikuwa nataka kujua mtihani ulikuwaje,” alisema huku mabinti zake wakicheka.
Kutokana na majibu yaliyokuwa yanatolewa na mabinti hao, baba yao alikuwa na ombi moja akiwaambia: “Mimi ninaomba mnifanyie kitu kimoja, kwa sababu sijawahi kutoka kwenye televisheni au gazeti hata siku moja. Sitaki kutoka nikiwa marehemu, naomba mnitoe ninyi.”
Baba yao alisema anaamini uwezo mkubwa kiakili walionao mabinti zake umetokana na mama yao, ambaye alianza kuwafundisha kusoma, kuandika na kusali tangu wakiwa wadogo nchini Uingereza walikozaliwa.
“Mama yao ni kichwa (ana akili) mimi nina akili zangu za kutengeneza hela na mambo mengine, lakini mama yao mwaka 2012 alipata Shahada ya Uzamili daraja la kwanza katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),” alisema huku akicheka.
Awali, wakati mwandishi wa gazeti hili akiingia nyumbani kwa Joyceline, alipokewa na mama mzazi, ambaye alionekana mwenye furaha kwa kuwa alikuwa amepewa taarifa ya ujio huo.
Kufaulu kwetu ni kawaida
Dada wa Sarafina Mariki aliyeshika nafasi na nne kitaifa, Benadetha alisema hakushtushwa na matokeo hayo ya mdogo wake kwa kuwa familia yao walijua angefaulu.
“Kuhusu kupata daraja la kwanza, tulijua tu hiyo ipo pale, lakini siyo kushika nafasi ya nne,” alisema na kuongeza kwamba: “Kwetu wote tunafanya vizuri katika masomo, daraja la kwanza, la pili ni kawaida, lakini huyu ameweka rekodi.”
Pia alisema tabia ya mdogo wake ya kupenda kusali imemfikisha alipo sasa: “Anapenda sana kusali, yaani yeye ndiye ambaye hutuamsha sisi watu wazima kwenda kanisani.”
Kwa upande wake Sarafina alisema tangu alipofahamishwa matokeo hayo ya mtihani ameshindwa kula chakula kwani hasikii njaa.
“Tangu niliposikia matokeo hayo jana (juzi) sijala chakula, sasa hivi inakaribia saa tisa mchana, ndiyo nitakula, ingawa sisikii njaa,” alisema.