Wazazi walalamika kupanda kwa bei za vifaa vya shule

Muktasari:

  • Baadhi ya wakazi wa Morogoro wamelalamikia ongezeko la bei ya vifaa vya elimu kwa ajili ya watoto wao wanaotarajia kufungua shule Januari 17, 2022.

Morogoro. Zikiwa zimebaki siku mbili shule za msingi na sekondari zifunguliwe wazazi na walezi wamelalamika kupanda bei kwa vifaa vya shule yakiwemo mashati ya shule, mabegi na viatu.

Wakizungumza na Mwananchi leo Januari 14, baadhi ya wazazi waliokuwa wakitafuta vifaa hivyo kwa ajili ya watoto wao wazazi hao walitaja vifaa vingine ni pamoja na magodoro, shuka, trakisuti na makwanja kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Mmoja wa wazazi hao, Hemed Seleman amesema kuwa uhitaji wa vifaa hivyo kwa katika kipindi hiki ni mkubwa hali inayowafanya wafabiashara wauze kwa bei kubwa ili wapate faida mara mbili.


"Kwa kweli wafanyabiashara wanauza bei za kutuumiza na kutukomoa, fedha niliyotoka nayo nyumbani imeisha na baadhi ya vifaa nimekosa," amesema Selemani.

Naye Flora Msangi alisema kuwa kila mfanyabiashara amekuwa akipanga bei zake na hivyo kuwafanya baadhi ya wazazi washindwe kumudu gharama hizo.

Flora amesema kuwa vipo baadhi ya vifaa vinavyoweza kupatikana kwenye mtumba kwa bei nafuu vikiwemo viatu na mabegi lakini vifaa kama magodoro na trakisuti havipatikani kwenye mitumba.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara walieleza sababu ya kupanda bei kwa vifaa hivyo na kudai kuwa inatokana na mahitaji kuwa makubwa hivyo upatikanaji wake viwandani umekuwa mdogo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao wa vifaa vya shule Esta Andrew amesema kuwa kupanda kwa bei kunatokana na hali ya upatikanaji wa vifaa hivyo viwandani na kwenye maduka ya jumla.

"Sisi hatuuzi bei ya kumkomoa mzazi kwa sababu hata sisi ni wazazi pia lakini kinachotokea ni kwamba kule kiwandani na kwenye maduka ya jumla tunakonunua nao wametupandishia bei," amesema Esta.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia viatu vya shule vikiuzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh25,000, mabegi Sh12,000 hadi Sh30,000, mashati ya shule Sh10,000 hadi Sh15,000, trakisuti Sh17,000 hadi Sh25,000.