Wazazi watajwa chanzo mmomonyoko maadili

Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dk Tumaini Katunzi akifungua mdahalo unaohusu mmomonyoko wa maadili nchini, uliofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Wazazi wametajwa kama miongoni mwa sababu za mmomonyoko wa maadili kufuatia wimbi la mmomonyoko wa maadili kuongezeka nchini.

Dar es Salaam. Wakati wimbi la maadili kumomonyoko likiendelea kushika kasi nchini, wazazi ni miongoni mwa vyanzo vilivyotajwa kupelekea mmomonyoko wa maadili nchini.

Wakizungumza katika mdahalo wenye mada 'Mmomonyoko wa Maadili Nchini' Jumatano Mei 3, 2023 katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, wawezeshaji na wachangia mada wamesema wazazi kutosimama imara katika kuwalea watoto ni miongoni mwa sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili nchini.  

Mwanasaikolojia Dk Charles Mwantepele amesema watu wengi huwalaumu watoto bila kujua kwamba maadili mabaya yanayooneka kwa watoto ni taswira ya wazazi wao kwani Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

"Wazazi wengi hawajitambui katika suala la malezi. Wazazi wako bize na mambo mengine na hawana muda kabisa na watoto wao, jambo ambalo sio rahisi kutambua mmomonyoko ulioko kwa mtoto," amesema Dk Mwantepele.
Pia Dk Mwantepele amesema baadhi ya maudhui yasiyo na maadili yanayorushwa na vyombo vya bahari yamechangia kwa asilimia kubwa mmomonyoko wa maadili katika jamii.

"Vyombo vya habari vikiamua kubadilisha maadili inawezekana. Sasa hivi vyombo vya habari vinapalilia maadili mabaya ikiwemo kupiga nyimbo zisizo na maadili zikiwa zenye jumbe za matusi na uvaaji usio na maadili," amesema Dk Mwantepele.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la KKKT changanyikeni Mchungaji Joshua Delem amesema kuna haja kubwa ya kujenga familia imara katika maadili, kwani familia imara kimaadili ndio itapelekea taifa imara lenye watu waadilifu.

"Hofu ya Mungu ikijengeka ndani yetu ni rahisi kuepuka kufanya matendo yasiyo yakimaadili. Kama hakuna hofu ya Mungu ndani ya mtu, ni rahisi shetani kumchezea anavyotaka," amesema Mchungaji Delem.

Kwa upande wake Imam wa Msikitiki wa Changanyike, Kaimu Amanzi amesema utandawazi umechangia sana maadili kumomonyoka kwa kiasi kikubwa.

Amanzi sasa hivi ni rahisi kukuta mtoto mdogo anamiliki simu ambayo anaweza kuona maudhui yasiyo na maadili ndani yake na kupelekea kumomonyoa maadili ya mtoto jambo ambalo huchangiwa na wazazi.

"Kila mtu kwa nafasi yake achukue hatua katika kufundisha maadili iwezekanavyo. Kama jamii ikishirikiana ni rahisi kuwa na jamii bora yenye maadili," amesema Amanzi.

Aidha amesema ni muhimu serikali kuweka sheria na kuzisimamia katika suala zima la maadili kwani sheria ikisimamiwa ipasavyo kuna nafasi kubwa ya kupunguza au kuondoa kabisa mmomonyoko wa maadili.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Afande Stella Mindasi amesema maadili yanapaswa kuzingatia jinsia na ni muhimu watoto kulelewa kulingana na jinsia zao akisema wazazi wengi hawajui namna gani ya kumlea mtoto wa kiume na wakike.

"Maadili ya kidini ni muhimu kuyazingatia kwani kanuni za kidini nyingi zinaingiliana na za serikali. Mfano kwenye dini unaambiwa usiibe kadharika sheria za nchi zinasema hivyo," amesema Afande Mindazi.

Aidha amewataka wahudhuriaji kutoa taarifa zozote zinazohusiana na ukatili wa kijinsia lakini pia matukio ya mmomonyoko wa maadili ikiwemo mapenzi ya jinsia moja.

Naye Magreth Hanga amesema suluhisho ni kila mzazi kuchukua hatua kujali suala la maadili kwa wale wanaowalea.

"Kama maadili yatasimamiwa kuanzia ngazi ya familia itasaidia kujenga msingi imara kwa watoto kuweza kupinga vitendo vya mmomonyoko wa maadili," amesema Hanga.