Waziri aeleza sababu wanyamapori kuvamia makazi ya watu

Muktasari:
- Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha maafa inatokana na shughuli za kibinadamu kufanyika katika njia wanazopita wanyama hao.
Morogoro. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha maafa inatokana na shughuli za kibinadamu kufanyika katika njia wanazopita wanyama hao.
Amesema hivi sasa matukio ya wanyama kuingia kwenye makazi ya watu yameongezeka na kutoa rai kwa watendaji wa wizara na hifadhi mbalimbali kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanalindwa.
“Mtendaji yeyote atakayehusika kuruhusu ama kuachia maeneo ya ushoroba (njia za wanyama) kuvamiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria. Yapo maeneo mengi ya mapito ya wanyamapori wakiwemo tembo ambayo yamezibwa kwa kujenga majengo, kufanya shughuli za kilimo na ufugaji na shughuli nyingine za kibinadamu.”
“Hata pale palipojengwa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero ni moja ya mapito ya tembo, maeneo haya ndio yanapovamiwa na wanyamapori wananchi wamekuwa wakiwafukuza wanyama hawa kwa fimbo kwa mazingira hayo lazima wapate madhara," amesema Dk Ndumbaro.
Kuhusu ombi la mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare la kupewa fidia kwa waliopata madhara kwa kuvamiwa na wanyamapori Dk Ndumbaro amesema Tanzania ndio nchi pekee inayotoa fidia kwa watu waliovamia maeneo ya hifadhi na kupata madhara.
Katika hatua nyingine, Ndumbaro amesema katika kuadhimisha siku ya wanyamapori Tanzania pia inasherehekea ushindi wa tuzo iliyoipata kutokana na hifadhi tatu zilizoingia kwenye hifadhi bora 25 duniani baada ya kushindanishwa na hifadhi nyingine.
Hifadhi hizo ni Serengeti ambayo imeshika nafasi ya kwanza duniani, nyingine ni hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro na Tarangire.