Waziri apiga marufuku utozaji ushuru kwa wauza dagaa Tunduma

Wednesday October 06 2021
ndakipic
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka maofisa Uvuvi kuacha kuwatoza ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi wafanyabiashara wanaouza  dagaa katika soko la ndani la Tunduma.

Waziri Ndaki amesema wafanyabiashara wanaopaswa kutozwa ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi, wale wanaonunua bidhaa hiyo na kuiza katika masoko ya nje ya Tanzania, hasa katika nchi za Zambia na Kongo.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 6, 2021 na wizara hiyo imeeleza kuwa Ndaki ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa dagaa katika mji wa Tunduma katika ziara yake ya siku mbili.

Kabla ya kutoa kauli hiyo wafanyabiashara hao walimweleza Ndaki kuwa wamekuwa wakitozwa ushuru wakati baadhi yao hawajishughulishi na uuzaji wa bidhaa hizo nje ya nchi.

"Tuache mara moja kuwatoza ushuru wafanyabiashara wa dagaa wanaoouza kwenye soko la ndani   katika mkoa wa Songwe kwa kigezo kuwa wote wanaziuza nje ya nchi,” amesema Ndaki.

Mbali na hilo, Ndaki amewawataka wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwa kufuata taratibu zilizowekwa na sambamba na kuacha tabia ya kutorosha dagaa kwa kutumia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru.

Advertisement

“Endapo mfanyabiashara atakamatwa kwa kosa la utoroshaji dagaa atanyang’anywa leseni, pamoja na mzigo wake na atafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi,” amesema Ndaki.

Awali mbunge wa Momba, Condester Sichalwe akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Tunduma, David Silinde, amesema wafanyabiashara wa dagaa katika soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe kutozwa ushuru wa usafirishaji mazao ya uvuvi nje ya nchini ni kero ya muda mrefu.

Advertisement