Waziri Aweso aitaka Dawasa kufikisha maji kwa wananchi

Muktasari:
- Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa na viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) wametembelea mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu.
Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametembelea na kukagua maboresho yaliyofanyika katika mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu na kutoa maagizo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuhakikisha wanafikisha maji kwa wananchi.
"Kwa kweli hali inaridhisha sasa, nilitoa maagizo ya maboresho katika mtambo huu, leo nimekuja kujionea, nitoe pongezi kwa menejimenti ya Dawasa kazi kubwa imefanyika hapa na katika chanzo tumekuta maji ya kutosha kabisa," amesema Aweso.
Waziri huyo ametembelea mtambo huo leo Alhamisi Julai 10, 2025 akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mwajuma Waziri pamoja na menejimenti ya Dawasa ikiongozwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Mkama Bwire.
Aweso ametoa maelekezo kwa Dawasa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji bila kikwazo chochote kwani hali ya mtambo ni nzuri na maji yapo yakutosha.

"Maji haya sasa ni wajibu wa Dawasa kuhakikisha yanawafikia wananchi na kunufaika nayo, Wizara itaendelea kuwapa ushirikiano kuhakikisha hamkwami, lakini pia ili kuboresha huduma Serikali imeshaagiza pampu mpya katika mtambo huu ili ziwe mbadala pale kunapotokea hitilafu," amesema Aweso.
Aweso ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Pwani pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushirikiano wa kutosha kwa wizara hali inayofanya huduma ya maji kuwa ya uhakika.
Kwa upande wa Mwajuma ameipongeza Dawasa kwa maboresho makubwa waliyofanya na kuwataka kuhakikisha wanawasikiliza wananchi ili kuondoa malalamiko, huku wakihakikisha wanapambana na upotevu wa maji kwa kudhibiti mivujo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon amesema wanashirikiana kwa karibu na Dawasa na Bonde Wami-Ruvu katika utafutaji wa vyanzo mbadala vitakavyosaidia kuzuia uharibifu katika chanzo cha mto Ruvu, ikiwemo ujenzi wa birika za kunyweshea mifugo katika vijiji vya Minazi Mikinda na Mpera-Mumbi.
Mhandisi Bwire amesema kwa mwaka huu wa fedha 2025 - 2026 Mamlaka imewekeza nguvu kubwa katika kuwaungia wananchi huduma ya maji ambapo imelenga kuunganisha wateja wapya 72,000.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amewataka watumishi wa Dawasa, kushirikiana na wananchi hususan wazee wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji.

Akizungumza kwenye kikao kati yake na watumishi wa mamlaka hiyo leo Alhamisi, amewasisitiza kuongeza bidii, mshikamano na uwajibikaji ili kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kufanikisha malengo ya Serikali katika sekta ya maji.
“Lengo letu kama Serikali ni kuhudumia wananchi, nanyi hakikisheni mnakuwa sehemu ya kufanikisha lengo hilo kwa kuhakikisha mnashirikiana ninyi kwa ninyi ndani ya taasisi na wananchi hususan wazee wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji,” ameelekeza Aweso.

Amesema wakishirikiana wao kwa wao ni rahisi kutoa huduma bora kwa wananchi kwani watakuwa wanazungumza lugha moja.