Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Bashungwa akunjua makucha miradi ya ujenzi kusuasua

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Issenye Wilaya ya Serengeti baada ya kukaguzi mradi wa ujenzi wa barabara ya Sanzate- Natta katika wilaya za Bunda na Serengeti yenye urefu wa kilomita 40. Picha na Beldina Nyakeke 

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku 14 kwa uongozi wa kampuni ya ukandarasi ya China Railways Seventh Group kufika ofisini kwake jijini Dodoma kujileza kwanini utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sanzate-Natta unaosuasua.

Serengeti. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku 14 kwa uongozi wa kampuni ya ukandarasi ya China Railways Seventh Group kufika ofisini kwake jijini Dodoma kujileza kwanini utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sanzate-Natta unaosuasua.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Jumatatu Oktoba 9, 2023 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha Wilaya za Bunda na Serengeti na kutokuridhishwa na kazi iliyofanyika hadi sasa.

"Mkandarasi huyu anatekeleza miradi mingine mitatu katika mikoa tofauti na anafanya kazi kwa kuzorota sana. Kila mradi uko nyuma  kwenye utekelezaji nah ii haikubaliki. Naagiza viongozi wakuu wa kampuni hii wafike wizarani kujieleza ndani ya siku 14 kuanzia leo Oktoba, 92023," amesema Bashungwa

Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mkurugenzi wa Miradi wa Tanroads, Boniface Mkumbo amemweleza Waziri Bashungwa kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 40 ulianza Julai 2020 na ulitarajiwa kukamilika Julai, 2022.

Hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh39.46 bilioni umefikia asilimia 47 pekee licha ya kutokamilika kwa takriban zaidi ya mwaka mmoja kwa mujibu wa mkataba.

"Tulibaini changamoto kadhaa ikiwemo uwezo mdogo wa kifedha wa mkandarasi, uwezo mdogo wa utendaji na wafanyakazi wasiokuwa na uzoefu tofauti na taarifa alizoziwasilisha wizarani wakati akiomba tenda. Lakini tayari tumekutana na mkandarasi na kumpa maelekezo kuhakikisha mradi unaendelea vizuri na utakamilika," amesema Mkumbo

Kutokana na taarifa hiyo, Waziri huyo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kutompa kazi mpya mkandarasi huyo pamoja na wengine wenye miradi maeneo mbalimbali nchini hadi miradi wanayotekeleza itakapofikia zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji.

"Kuanzia sasa hakuna kumpa kazi mpya mkandarasi kama mradi alionao hajafikisha asilimia 60….hakuna kumrundikia mkandarasi mmoja kazi nyingi kwa sababu hii ni miongoni mwa sababu za wengi kushindwa kutekeleza na kukamilisha miradi kwa wakati," ameagiza Bashungwa

Ametaja mradi mwingine unaotekelezwa na mkandarasi huyo kuwa ni ujenzi wa barabara ya Kibaoni- Mlele Mkoa wa Katavi yenye urefu wa kilomita 50 ambapo hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 11 badala ya asilimia 42 kama ilivyopaswa kuwa kwa mujibu wa mkataba.

Mradi mwingine ni ujenzi wa barabara ya Amani- Luanda mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilomita 35 ambao umetekelezwa kwa asilimia 22 badala ya asilimia 84.

Mkandarasi huyo pia anatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 33.7 eneo la Utete Rufiji ambao pia utekelezaji wake uko nyuma.

Diwani wa Kata ya Issenye, Nyarobi Nyarobi ameiomba Serikali kuongeza usimamizi kwenye utekelezaji wa miradi ili siyo tu ikamilike kwa wakati, bali pia kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha za umma zinazotumika kuitekeleza.