Waziri Biteko atoa neno mkataba GGML, Stamico wa Sh55.2 bilioni

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Elder Damon (kushoto) akisaini mkataba kati ya kampuni hiyo na Shirika la Madini la Taifa Stamico) wenye thamani ya Sh55.2 bilioni kwa lengo la kuendeleza shughuli za uchorongaji miamba kwenye migodi ya kampuni hiyo. Kulia na Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse.

Muktasari:

  • Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) zimeingia mkataba 55.2 bilioni huku Waziri wa Madini, Dk Deto Biteko akizitaka kampuni zingine za ndani kunufaika na zabuni za nje zinapotangazwa.

Dodoma. Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Shirika la Madini la Taifa (Stamico), imesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh55.2 bilioni kwa lengo la kulipatia shirika hilo kandarasi ya kuchoronga miamba ndani ya mgodi wa GGML.

 Akizungumza katika hafla fupi ya kutia saini makubaliano hayo jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Elder Damon alisema tangu kuanzishwa kwa kanuni za ushirikishaji wazawa kwenye shughuli za uchimbaji madini mwaka 2018, idadi ya wafanyabiashara watanzania waliofanikiwa kushinda kandarasi mbalimbali ndani ya mgodi huo, imeongezeka.

 "Nia yetu imekuwa kusaidia jamii kwa kuwapa ujuzi ili kuwawezesha kushindana kikamilifu. Stamico imekuwa ikitoa huduma za uchorongaji miamba ndani ya GGML, kusaidia programu za uchimbaji wa wazi tangu Septemba 2020.”

 “Stamico imetoa huduma za uchorongaji miamba kwa viwango vya juu kwa kuzingatia usalama na ufanisi katika sekta ya uchimbaji madini kulingana na malengo ya sekta hii. Makubaliano haya na Stamico yanaonyesha uungaji mkono unaoendelea katika ukuzaji wa ujuzi na utaalamu kuhusu uchorongaji miamba na utafiti wa madini nchini,” alisema Damon.

 Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse aliipongeza GGML kwa imani waliyoionesha kwao tangu walipoanza kufanya kazi mwaka 2020.

 “Tunapenda kuwahakikishia GGML na Serikali kuwa kazi yetu itatekelezwa kwa ubora na viwango vya juu,” alisema Dk Mwasse.

 Mgeni rasmi aliyehudhuria hafla ya utiaji saini, Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko alisema hali ya Stamico imebadilika na kuwa bora zaidi tangu mkataba wao wa awali na Geita Gold Mining Limited ulipoanza.

 “Tangu 2020 Stamico iliposaini mkataba wake wa kwanza na GGML, mambo yameboreshwa ndani ya Shirika. Stamico imefanya vizuri sana kwa kuzingatia ubora na ufanisi wa kazi jambo ambalo wengi wetu tunajivunia.

 “STAMICO imeiwakilisha vizuri nchi yetu ndiyo maana wawekezaji wengi kama GGML bado wana imani ya kufanya nao kazi,” alisema Dk Biteko.

 Aidha, Dk Biteko alizitaka kampuni nyingine za ndani kunufaika na zabuni za nje kila zinapotangazwa kwa sababu kanuni za sheria hiyo ya madini ya mwaka 2017 zinatoa nafasi kwa watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye sekta ya madini.