Waziri Jafo, wenzake watatu kikaangoni bungeni wiki hii

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo

Muktasari:

  • Wizara wanazozisimamia zinakabiliwa na masuala ambayo kwa siku za karibuni yamekuwa yanahojiwa ama na wabunge au na wananchi.

Dodoma. Wakati Bunge la Bajeti likitarajia kuendelea na vikao vyake kesho, wiki hii mawaziri watatu wanatarajiwa kuwekwa kikaangoni pale watakapowasilisha makadirio na matumizi ya wizara zao kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Hata hivyo, macho na masikio ya Watanzania, yataelekezwa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) inayoongozwa na Dk Selemani Jafo, ambaye atalazimika kujibu hoja za wabunge kutokana na mambo kadhaa yaliyojitokeza nchini.

Kwa miaka ya nyuma hoja kubwa katika wizara hiyo zilitawaliwa na masuala ya Muungano, lakini safari hii kuna uwezekano mkubwa kuibuka suala la mazingira, hasa uchafuzi wa Mto Mara.

Wakizungumza na Mwananchi jana jijini Dodoma, baadhi ya wabunge wamesema wizara hiyo imebeba hoja nyingi zinazowagusa wananchi na kuhitaji majibu ya kina kutoka kwa waziri mwenye dhamana.


Ripoti ya Mto Mara

Suala la Mto Mara limeibuliwa na Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara akisema tangu wabunge walipoikataa ripoti ya uchafuzi huo na Serikali kuahidi kuunda kamati nyingine itakayofanya uchunguzi upya, bado haijaelezwa hadi sasa imefanya kitu gani.

“Tunasubiri kesho (leo) kama itakuwepo katika hotuba ya bajeti yake (Waziri wa Mazingira, Selemani Jafo), ndiyo tutaanzia hapo,” alisema Waitara huku akibainisha kuwa kwa sasa yuko jimboni kwake Tarime Vijijini ulipo mgodi huo.

Kauli hiyo ya Waitara inaungwa mkono na Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo aliyesema wizara hiyo inapaswa ije na majibu ya kuridhisha kwa kuwa mbali ya uchafuzi wa Mto Mara, pia kuna suala la mgogoro wa Hifadhi ya Ngorongoro.

Profesa Kitila alisema hoja hizo mbili ambazo kwa nyakati tofauti zimezua mjadala mkali katika vikao vya wabunge, bado hazijapata majibu mapaka sasa.

“Hivyo, katika hili wabunge na wananchi tutahitaji majibu ya kina katika haya masuala,” alisema Dk Kitila.

Kauli za wabunge waliopata kuwa mawaziri katika awamu ya tano na sita, zinaashiria namna gani mjadala mkubwa utahusu ripoti ya timu zilizoundwa kuchunguza uchafuzi wa mto huo.

Suala hilo liliibua maswali mengi kutoka kwa wananchi na hata Kamati ya Bunge ya Mazingira ambayo iligoma kuipokea ripoti husika, ikiwa ni siku chache kabla ya Bunge la Bajeti kuanza vikao vyake.

Kwa upande wa Ngorongoro, kuna suala la kuhamisha baadhi ya wakazi kama sehemu ya kulinda uhifadhi, ambalo limekuwa likilalamikiwa.

Wakati wabunge hao wakiyasema hayo, tayari kuna taarifa nyingine za uchafuzi uliotokea kwenye bomba la maji linalodaiwa kuwa na maji hatarishi kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.

Bomba hilo linalodaiwa kupasuka katika Kijiji cha Nyagoto wilayani Tarime na kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo, vilevile linaweza kuwa sehemu ya mjadala huo bungeni.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 4 asubuhi na kumlazimu mbunge wa jimbo la Tarime vijijini, Waitara kufika kwenye eneo la tukio ili kujionea hali halisi, huku maofisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na waziri wa madini wakichukua hatua kadhaa.

Wizara hiyo iliyopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais imepewa siku moja kuwasilisha, kujadili na kuhitimisha makadirio yake kwa mwaka wa fedha 2022/23.


Wizara nyingine

Ratiba ya Bunge inaonyesha baada ya Wizara ya Muungano na Mazingira, itafuatiwa na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imepangiwa siku moja ya Aprili 27, 2022.

Wizara ya Katiba na Sheria miongoni mwa hoja ambazo zinatarajiwa kuibuka ni madai ya Katiba mpya na sheria zinazohitaji kufanyiwa marekebisho.

Baada ya hapo wabunge watapokea makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini ambayo nayo itajadiliwa kwa siku moja Aprili 28, 2022.

Miongoni mwa hoja ambazo zinatarajiwa kuibuka katika mjadala wa Wizara ya Madini ni kuhusu jiwe la rubi lililotangazwa kuwa na uzito wa kilo 2.8 lenye thamani ya Sh276 bilioni ambalo lilitarajiwa kupigwa mnada Dubai, Falme za Kiarabu.

Aprili 29, 2022 na Mei 4, 2022 wabunge watajielekeza kwenye mjadala wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo nayo inatarajiwa hoja kubwa itahusu utendaji wa Jeshi la Polisi ambao unalalamikiwa na Watanzania wengi.

Machi 11 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya CCM ilielekeza Serikali kuangalia upya mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini ambao umekuwa hauridhishi kutokana na kulalamikiwa na wananchi.

Siku chache baada ya malalamiko hayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alilieleza gazeti hili katika mahojiano maalumu kuwa atalifanyia marekebisho kidogo jeshi hilo.