Waziri Mkenda amlilia Mramba
Muktasari:
- Mbunge wa jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Basil Mramba kilichotokea leo Jumanne Agosti 17, 2021 jijini Dar es Salaam.
Rombo. Mbunge wa jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema amepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Basil Mramba kilichotokea leo Jumanne Agosti 17, 2021 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Profesa Mkenda amesema Mramba alitumia nafasi yake ya ubunge kujenga na kuendeleza Wilaya ya Rombo kwa miaka 20 ya ubunge wake na kusema atakumbukwa kwa mengi.
"Sisi wana Rombo tutamkumbuka Mramba kwa mengi na hatutasahau kamwe maendeleo aliyotuletea," amesema Profesa Mkenda
Soma zaidi:Basil Mramba afariki dunia kwa Uviko-19
"Historia ya Maisha wasifu na haiba yake vilitosha kumfanya kuwa ni kiongozi wa kutegemewa na sisi sote hata baada ya kuondoka kwenye nafasi rasmi ya uongozi wa kisiasa, tumempoteza kiongozi shupavu ,mwenye busara ,mvumilivu na muungwana,"
Mkenda amesema Mramba ambaye aliwahi kuwa katika wizara mbalimbali atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka.
"Kati ya mambo ambayo Mramba atakumbukwa nayo ni juhudi zake za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchni, wengi tutamkumbuka jinsi akiwa Waziri wa fedha aliondoa kodi na tozo ambazo zilikuwa kero kwenye uchumi wetu," amesema Waziri Mkenda.