Basil Mramba afariki dunia kwa Uviko-19

Basil Mramba afariki dunia kwa Uviko-19

Muktasari:

  • Aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba amefariki dunia leo Jumanne Agosti 17, 2021 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba amefariki dunia leo Jumanne Agosti 17, 2021 jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa Uviko-19 (corona).

Taarifa iliyotolewa na mwanaye,  Godfrey Mramba imeeleza kuwa baba yake amekutwa na umauti leo asubuhi wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Regency.

“Mzee amezaliwa Mei 15, 1940, amefariki mapema leo Agosti 17, ameugua pale Regency Medical Centre muda wa wiki mbili, amepata maradhi ya Covid 19 tumempoteza leo, tunamshukuru Mungu kwa maisha yake na tutayasherehekea,” amesema Godfrey alipozungumza na Mwananchi kwa simu. 

Hata hivyo, Godfrey ameweka wazi kuwa kutokana na janga la Uviko 19 msiba huo utahusisha watu wa familia pekee ili kuepuka mkusanyiko.

“Kutokana na janga hili familia inapokea salamu za pole, faraja na sala zenu ila tutaomba shughuli za msiba uwahusishe wanafamilia pekee na tutakuwa nyumbani kwa marehemu barabara ya Mawenzi Oysterbay,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Godfrey.