Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru yaokoa Sh116 milioni, mfumo wa NeST wasaidia

Kamanda wa PCCB Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata, akihutubia mkutano na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa PCCB Tanga kwa kipindi cha January hadi Mach 2026. Picha na Mbonea Herman.

Muktasari:

  • Katika Shule ya Sekondari Chongoleani, ujenzi wa madarasa mawili na vyoo ulikuwa umekwama licha ya fedha kutolewa tangu Machi 2024.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuiana na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imebainisha kuwa mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (NeST) umeibua dosari katika utekelezaji wa miradi ya elimu mkoani Tanga na kufungua njia ya kuokolewa kwa zaidi ya Sh116.2 milioni.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata ametoa kauli hiyo leo Juni 8, 2026 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya utendaji kazi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.

Amesema ufuatiliaji wa miradi hiyo umebaini upungufu uliokuwa ukichelewesha utekelezaji licha ya fedha kutolewa.

“Tumebaini dosari kupitia mifumo ya ununuzi na kuchukua hatua mapema, jambo lililosaidia kuzuia upotevu wa fedha za umma,” amesema Ndwata.

Katika Shule ya Sekondari Chongoleani, ujenzi wa madarasa mawili na vyoo ulikuwa umekwama licha ya fedha kutolewa tangu Machi 2024.

Takukuru ilibainika kuwa makadirio ya gharama za madarasa yalikuwa chini ya bei ya soko na kufanya zabuni kukataliwa na mfumo wa NeST.

Kwa upande wa vyoo, hakukuwa na maandalizi ya makadirio ya gharama, hali iliyosababisha taratibu za manunuzi kushindwa kuanza kabisa.

“Baada ya kubaini changamoto hizo, tuliimarisha uwajibikaji na sasa mradi unaendelea vizuri,” amesema Ndwata.

Katika hatua nyingine, Takukuru ilifuatilia mradi wa Shule ya Sekondari Kwabastola wilayani Muheza, wenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Ndwata amesema katika mradi huo, milango ilipakwa varnish, mikanda ya gypsum ikarekebishwa na vitanda 57 kununuliwa vyenye thamani ya Sh22.4 milioni.

“Tunafuatilia pia ukamilishaji wa sakafu, uwekaji wa vigae na ununuzi wa vitanda vilivyobaki ili wanafunzi wanufaike kikamilifu,” amesema Ndwata.

Akizungumzia uelimishaji umma, kamanda huyo wa Takukuru amesema wamewafikia wananchi 189,521 kupitia semina, mikutano ya hadhara, klabu za wapinga rushwa, maonyesho na vipindi vya redio.

Kuhusu uchunguzi, Ndwata amesema jumla ya malalamiko 133 yalipokelewa ambapo 100 yalihusu rushwa na mengine kushughulikiwa kwa ushauri au kuhamishiwa taasisi husika.

“Tumefungua mashauri 11 na jumla ya mashauri 18 yanaendelea mahakamani huku tukihakikisha haki inatendeka,” amesema Ndwata.

Kwa upande wa mikakati ya Aprili hadi Juni 2026, Kamanda huyo wa Takukuru amesema wataendelea kuimarisha uelimishaji, uchambuzi wa mifumo na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma.