Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Adakwa akituhumiwa kujifanya ofisa wa Takukuru Arusha

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo wakati akithibitisha tukio hilo leo Jumapili Juni 7, 2026.

Muktasari:

  • Mtuhumiwa alikamatwa Juni 3, 2026 katika Hoteli ya Briston jijini Arusha baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na raia wema.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha inamshikilia Ashley Mrangi (48), mkazi wa eneo la Kwa Morombo, kwa tuhuma za kujifanya ofisa wa taasisi hiyo na kutumia utambulisho huo kwa lengo la kujipatia manufaa kinyume cha sheria.

Akithibitisha tukio hilo leo Jumapili Juni 7, 2026, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema mtuhumiwa alikamatwa Juni 3, 2026 katika Hoteli ya Briston jijini Arusha baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na raia wema.

Ngailo amesema kosa la kujifanya ofisa wa Takukuru ni kinyume cha Kifungu cha 36 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya Mwaka 2023.

Amesema kabla ya kukamatwa kwake, taasisi hiyo ilipokea taarifa mtuhumiwa alikuwa akijitambulisha kwa wananchi kuwa ni ofisa wa Takukuru na kutumia madai hayo kuwashawishi baadhi ya watu kuwa ana uwezo wa kuingilia au kushawishi mwenendo wa uchunguzi unaoendelea ndani ya taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Ngailo, mtuhumiwa alikutana na mmoja wa wananchi aliyekuwa akichunguzwa na Takukuru Mkoa wa Arusha na kujitambulisha kwake kama ofisa wa taasisi hiyo.

“Inadaiwa alimweleza mwananchi huyo kuwa anafahamu kuhusu tuhuma zinazomkabili na alikuwa tayari kumsaidia ili suala hilo lisifike hatua zaidi za uchunguzi. Pia alimhakikishia kuwa angemsaidia kurejeshwa kwa mali zilizokuwa zikishikiliwa katika mchakato wa uchunguzi,” amesema Ngailo.

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo, Takukuru iliandaa operesheni maalumu iliyowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa akiwa hotelini hapo akisubiri kukutana na mtoa taarifa kwa hatua zaidi za utekelezaji wa makubaliano yao.

Ngailo amesema upelelezi wa awali umebaini viashiria vya uwezekano wa kuwapo kwa ushirikiano kati ya mtuhumiwa huyo na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kutoka taasisi mbalimbali za umma.

“Upelelezi unaendelea ili kubaini watu wengine waliohusika au walionufaika na vitendo hivyo, pamoja na mazingira yaliyomwezesha mtuhumiwa kupata taarifa za ndani zinazohusu uchunguzi wa taasisi,” amesema.

Ameongeza kuwa taratibu za kisheria zinaendelea kukamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Wakati huohuo, Takukuru imewataka wananchi kuwa makini dhidi ya watu wanaojitambulisha kama maofisa wa taasisi hiyo au watumishi wa umma kwa lengo la kujipatia fedha au manufaa mengine kwa njia zisizo halali.

Ngailo amewahimiza wananchi kutoa taarifa mara moja wanapokutana na matapeli wa aina hiyo ili hatua za haraka za kisheria ziweze kuchukuliwa.

“Nawahakikishia wananchi kuwa tutaendelea kushirikiana nao katika kupambana na rushwa na vitendo vyote vya udanganyifu vinavyohujumu utawala wa sheria. Wananchi wanaweza kufika katika ofisi zetu au kutumia namba ya bure 113 kutoa taarifa,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa Arusha, Elizabeth Joseph, amesema hatua iliyochukuliwa na Takukuru itasaidia kupunguza vitendo vya utapeli vinavyoongezeka jijini humo.

“Hatua hii itatoa funzo kwa watu wanaotumia majina ya taasisi za umma kujipatia fedha kwa njia zisizo halali na kuwahamasisha kutafuta njia halali za kujipatia kipato,” amesema.