Udanganyifu wa kidijitali waibua tahadhari Serikali
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dk Rahma Salim Mahfoudh, akizungumza leo Jumatatu Juni 8, 2026 katika Jukwaa la Uhamasishaji Dhidi ya Udanganyifu katika Sekta ya Umma lililoandaliwa na Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu (ACFE) Tanzania, linalofanyika jijini Arusha.
Muktasari:
- Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Kenneth Nindie, amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma ili kuongeza uwajibikaji na kuziba mianya ya ubadhirifu.
Arusha. Serikali imezitaka taasisi za umma na binafsi kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na kutumia teknolojia za kisasa kukabiliana na ongezeko la udanganyifu wa kifedha unaofanywa kupitia mifumo ya kidijitali, ikionya kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha uchumi wa taifa na kudhoofisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 8, 2026 na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dk Rahma Salim Mahfoudh, wakati akifungua Jukwaa la Uhamasishaji Dhidi ya Udanganyifu katika Sekta ya Umma (Public Sector Fraud Awareness Forum) lililoandaliwa na Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu (ACFE) Tanzania.
Dk Mahfoudh amesema maendeleo ya teknolojia na mifumo ya kifedha yameleta manufaa makubwa, lakini wakati huohuo yamefungua milango ya aina mpya za udanganyifu ambazo ni ngumu zaidi kugundua na kudhibiti.
Amesema taasisi zinapaswa kutumia mbinu za kisasa za kuzuia, kugundua na kuchunguza udanganyifu ikiwemo uchambuzi wa taarifa (data analytics), uchunguzi wa kitaalamu wa kifedha (forensic accounting) na uchunguzi wa kidijitali (digital forensics).
“Miaka michache iliyopita tulikuwa tunazungumzia udanganyifu wa kawaida unaofanywa na mtu mmoja mmoja. Leo tunashuhudia udanganyifu unaofanywa kwa kutumia mitandao ya kimataifa, teknolojia za kisasa na mifumo ya kidijitali inayohitaji maandalizi makubwa ili kuudhibiti,” amesema.
Rais wa Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu (ACFE) Tanzania, Ali Mabrouk Juma, akizungumza katika Jukwaa la Uhamasishaji Dhidi ya Udanganyifu katika Sekta ya Umma, jijini Arusha leo Jumatatu Juni 8, 2026.
Amesema endapo mianya ya udanganyifu, rushwa na ubadhirifu itaendelea kuongezeka, athari zake hujitokeza moja kwa moja katika uchumi wa taifa na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
Dk Mahfoudh ametaja moja ya changamoto mpya inayoongezeka duniani kuwa ni mfumo unaojulikana kama Fraud as a Service, ambapo wahalifu huuza teknolojia, taarifa na utaalamu wa kufanya udanganyifu kwa watu wengine kwa malipo.
“Kuna wanaouza programu za kufanya ulaghai, wengine huuza taarifa zilizoibiwa za watu na wengine hufanya mashambulizi ya kimtandao kwa niaba ya wahalifu walioko nyuma ya matukio hayo. Mfumo huu umefanya uhalifu wa kifedha kuwa rahisi zaidi kutekelezwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mahfoudh, hali hiyo imeongeza hatari kwa taasisi za umma, taasisi za kifedha, mifumo ya malipo, mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni za bima na mashirika mengine kutokana na urahisi wa upatikanaji wa zana za kufanya uhalifu wa kifedha.
Ametaja baadhi ya matukio yanayoongezeka kuwa ni ulaghai katika mifumo ya malipo ya kidijitali, mashambulizi ya kimtandao, wizi wa utambulisho, matumizi mabaya ya akili mnemba (AI), kughushi nyaraka na uhamishaji wa fedha kwa kutumia taarifa za uongo.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya udanganyifu hayapaswi kuachwa kwa wakaguzi pekee, bali yanahitaji usimamizi wa kimkakati kutoka ngazi za juu za taasisi na kupewa uzito sawa na usimamizi wa fedha, rasilimali watu na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Awali, Rais wa ACFE Tanzania, Ali Mabrouk Juma, amesema dunia inakabiliwa na ongezeko la udanganyifu wa kisasa unaotumia teknolojia na mifumo ya kidijitali, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi mbalimbali.
Amesema ACFE Tanzania inaendelea kutoa mafunzo, tafiti na miongozo ya kitaalamu inayolenga kuimarisha uwezo wa taasisi kuzuia na kudhibiti udanganyifu pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wenye hadhi ya Certified Fraud Examiner (CFE).
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Mhandisi Kenneth Nindie, amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma ili kuongeza uwajibikaji na kuziba mianya ya ubadhirifu.
Hata hivyo, amesema moja ya changamoto kubwa inayokabili sekta ya ukaguzi wa ndani ni ugumu wa kupata ushahidi unaokubalika kisheria licha ya kubainika kwa viashiria vya ubadhirifu, jambo linalofanya baadhi ya kesi kushindwa kufikia hatua zinazotarajiwa katika vyombo vya sheria.
Amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani kupitia mafunzo na vyeti vya kitaalamu vya uchunguzi wa udanganyifu ili kuwawezesha kufanya uchunguzi unaokidhi viwango vya kitaalamu na mahitaji ya kisheria.