Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Mkuu aagiza ujenzi wa barabara mbili Mufindi

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na wananchi wa Idofi, Makambako mkoani Njombe, alipoanza ziara yake ya kikazi leo Mei 2, 2026 katika mikoa ya Iringa na Njombe.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba ametoa agizo hilo leo katika ziara yake aliyoifanya Igowole Mufindi mkoani Iringa, huku akisema hatua hiyo ni kuhakikisha barabara zinapitika na magari ambayo hubeba mazao mbalimbali yanapita bila shida ili kukuza uchumi.

Iringa.‎ Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa barabara katika barabara ya Mtwango- Nyololo na Mafinga -Mgololo kwa kiwango cha lami Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo haupaswi kucheleweshwa kwa kisingizio chochote kwani wananchi wanahitaji matokeo ya haraka.

Amesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za uzalishaji na viwanda, hivyo kuchelewa kwake kunawaathiri wananchi moja kwa moja katika shughuli zao za kila siku.

‎Akizungumza leo Mei 2, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Igowole Mufindi mkoani Iringa Dk Mwigulu amesisitiza kwa msisitizo mkubwa kuwa ahadi na maagizo yanayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan siyo ya kupuuzwa wala kucheleweshwa, bali yanapaswa kupewa uzito unaostahili na kusimamiwa ipasavyo.

“Kama Rais ameelekeza au ameahidi jambo, hayo ni maelekezo kamili na si vinginevyo hivyo watendaji hakikisheni mnatekeleza kwa wakati bila visingizio,” amesema, Dk Mwigulu akiongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.

‎Katika kusukuma mbele utekelezaji huo, Mwigulu Nchemba ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa kuhakikisha mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara unakamilika ndani ya muda mfupi, akitoa muda wa wiki mbili kupata mrejesho wa hatua zilizofikiwa.

‎Aidha, amemwelekeza Mkuu wa Mkoa huo, Kheri James kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, akimtaka kutumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara kuhakikisha kila hatua inafanyika kwa wakati na kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanroads mkoani Iringa, Mhandisi Hosea Mashaka ameeleza kuwa mchakato wa zabuni unaweza kuchukua hadi wiki tatu, lakini Dk Mwigulu amesisitiza kuwa kasi iongezwe ili wananchi waanze kuona utekelezaji halisi wa mradi huo.

‎Kuhusu miradi iliyokwama kwa muda mrefu, Waziri Mkuu ameagiza hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo kuandika barua kwenda makao makuu ya Tanroads ili kuharakisha maamuzi.

“Sitaki kuona miradi inakaa bila sababu za msingi andikeni barua leo na ifikapo Jumatatu nipate nakala ili hatua zichukuliwe mara moja,” amesema kwa msisitizo, akionyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.

‎Naye Mbunge wa Mufindi Kusini na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema barabara ya Nyororo–Igowole ni muhimu kwa uchumi wa taifa kutokana na uwepo wa viwanda zaidi ya 25 vinavyotegemea miundombinu hiyo.

Hata hivyo, amelalamikia ubovu wa barabara hiyo akisema mara nyingi huwa na mashimo na matengenezo yake hufanyika kwa muda mfupi tu wakati wa ziara za viongozi.

"Watu wa Mufindi ukiuliza wanataka nini basi moja ni barabara,mbili barabara,tatu barabara,nne barabara na tano ni barabara na bado ombi letu kubwa litakuwa ni barabara," amesema Kihenzile

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais -Tamisemi, Dk Festo Dugange amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kutoka Sh4 bilioni mpaka Sh58 bilioni kwaajili ya barabara za Mufindi na pia barabara zimeendelea kuongezwa kutoka kilomita 216 kilomita 311.

"Na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi inajua kuwa Sh 9 bilioni zinahitajika kuboresha barabara Wilayani Mufindi ambazo zimeharibika kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu," amesema Dk Dugange.

‎Aidha kauli hizo zimeibua matumaini mapya kwa wananchi wa Mufindi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara inayowaathiri katika shughuli za usafirishaji wa mazao na bidhaa.

‎Baadhi ya wananchi wa Mufindi wamepongeza agizo la Mwigulu Nchemba wakisema ni hatua muhimu inayoweza kuboresha uchumi wa eneo hilo na kurahisisha usafiri wa bidhaa na huduma.

Wananchi wengine wamesema wamekuwa wakisikia ahadi za ujenzi wa barabara kwa muda mrefu bila kuona utekelezaji wake, hivyo wanatarajia safari hii kutakuwa na mabadiliko ya kweli.

“Tumechoka na ahadi zisizotekelezwa; tunataka kuona mashine zinaanza kazi haraka,” amesema mkazi mmoja wa Igowole.

Wapo pia waliobainisha kuwa ubovu wa barabara umekuwa ukisababisha ajali na uharibifu wa vyombo vya usafiri, hali inayoongeza hasara kwa wananchi na wamesema ujenzi wa barabara hiyo utakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto hizo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameitaka serikali kuhakikisha usimamizi wa karibu unafanyika ili kuzuia ubadhirifu wa fedha na kuhakikisha ubora wa barabara unazingatiwa.

“Sio tu kujenga, bali tujenge barabara imara itakayodumu kwa muda mrefu,” amesema mwananchi mwingine ambaye jina lake hakutaka kujulikana,” amesema.