Waziri Mkuu Majaliwa kutua Kilimanjaro kwa ziara ya siku mbili

Monday September 20 2021
majaliwa pc
By Janeth Joseph

Moshi. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kufanya ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro ambapo atazindua na kutembelea miradi mbalimbali pamoja na kuweka jiwe la msingi katika stendi ya mabasi ya Kimataifa ya Ngangamfumuni ambapo itagharimu zaidi ya Sh20 bilioni.


Hayo yamesemwa leo Septemba 20, 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema Waziri Majaliwa atawasili mkoani humo Septemba 22 na kuanza ziara yake Septemba 23 na 24, 2021.


Akiwa mkoani humo Waziri Mkuu Majaliwa atafungua  kiwanda cha pombe kali cha Serengeti kilichopo Manispaa ya Moshi pamoja na kutembelea kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga ambacho kimegharimu Sh136 bilioni ambapo tayari kimeshaanza uzalishaji.


Amesema pia atatembelea mradi mkubwa wa maji wa Mwanga - Same -Korogwe ambao utanufaisha mamia ya wananchi mkoani humo.


"Niwaombe wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro mjitokeze kwa wingi kwenye huu ujio mzito wa kiongozi wetu ambapo atatembelea maeneo mbalimbali pamoja na kufanya mikutano ya hadhara, niwaombe mjitokeze kwa wingi kumsikililiza," amesema RC Kagaigai.


Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi mkoani humo kuendelea kuchukua tahadhari za ugonjwa wa Uviko- 19 pamoja na kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo.

Advertisement
Advertisement