Waziri Mwigulu kubana matumizi magari ya viongozi

Muktasari:

  • Waziri amekuwa akirudia mara kwa mara kuhusu kauli hiyo akisema viongozi wenye sifa ya kukopeshwa magari wanaweza kukopeswa ili yawe mali yao kwa madai ni njia mojawapo ya kubana matumizi.

Dodoma. Serikali imerudia kauli yake kuhusu kubana matumizi ya magari kwa watumishi na kusisitiza viongozi wenye sifa watakopeshwa magari.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asia Halamga ambaye ametaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya GPSA kuchelewesha ununuzi a magari ya Serikali.

Kwenye swali la msingi mbunge huyo ameomba kujua ni namna gani Serikali inaweza kuagiza magari moja kwa moja kutoka Toyota Japan badala ya kununua kupitia kwa mawakala ambao wamekuwa wakisababisha fedha nyingi kutumika.

Waziri Mwigulu amesema ili kupunguza gharama, ni kuweka utaratibu wa kuwakopesha magari watumishi wenye sifa za kukopa ili kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo ya magari kwa kuwakopesha viongozi wenye sifa.

“Mtazamo wa Serikali ni kuendelea kupunguza masuala ya matumizi ya magari na kwenye mpango wa bajeti tumekuja na utaratibu wa watumishi wenye sifa kukopa magari ili yawe ya kwao kwa ajili ya kuipunguzia Serikali ghamata za uendeshaji,” amesema Dk Mwigulu.

Kuhusu ucheleweshaji, Naibu Waziri amesema, ucheleweshaji wa ununuzi wa magari Serikalini umekuwa ukisababishwa Mabadiliko ya aina (models) za magari yanayotumiwa na Serikali ambapo upatikanaji wa aina mpya huweza kuchukua muda mrefu zaidi kutegemea na idadi ya mahitaji kwa Serikali.

Nyingine ni athari za kiuchumi zinazoathiri mnyororo wa uzalishaji na usafirishaji mfano UVIKO-19, iliyopelekea viwanda vinavyozalisha vipuri vya magari kufungwa na kupelekea changamoto ya uhaba wa vifaa vya Tehama ambavyo kwa sehemu kubwa ya magari ya kisasa hutumia teknolojia kubwa ya umeme na changamoto ya usafirishaji wa magari, ikiwemo uhaba wa wasafirishaji na ukosefu wa makasha ya kusafirisha mizigo.

Hata hivyo amesema kwa sasa mnyororo wa ununuzi wa magari duniani umeanza kuimarika na magari yote yanafika kwa wakati na kukabidhiwa kwa taasisi zilizoagiza lakini akaeleza kuwa hali ya ya upatikanaji wa magari kwa wakati imerejea.

Kuhusu kuagiza moja kwa moja kwa Toyota Japan, amesema mfumo unalitambulia hilo lakini maofisa manunuzi wanaruhusiwa kwa mujib wa sheria kuagiza magari moja kwa moja au kupitia kwa wakala.