Waziri mwingine wa Magufuli akumbwa na sakata la Madini

Wajumbe wa Kamati Maalumu iliyoundwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kuchunguza biashara ya tanzaniate wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia baada ya kukabidhiwa taarifa hiyo katika halfa iliyofanyika kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

Ripoti ya kamati hiyo iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuangalia mfumo wa uchimbaji, udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini hayo ya vito, jana ilikabidhiwa kwa mkuu huyo wa chombo hicho cha kutunga sheria na baadaye kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Dar es Salaam. Ripoti iliyoelezewa kuwa ni “ya kusikitisha” kuhusu madini ya almasi na tanzanite, imewataja tena mawaziri wawili wa zamani na wengine wawili wa sasa kuhusika katika dosari zinazosababisha nchi kupoteza fedha nyingi.

Ripoti ya kamati hiyo iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuangalia mfumo wa uchimbaji, udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini hayo ya vito, jana ilikabidhiwa kwa mkuu huyo wa chombo hicho cha kutunga sheria na baadaye kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Leo, ripoti hiyo itakabidhiwa kwa Rais John Magufuli, ambaye alichukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kutengua uteuzi wa Profesa Muhongo baada tu ya kukabidhiwa ripoti ya makinikia.

Waliotajwa katika ripoti hiyo ni mawaziri wawili wa zamani, Profesa Sospeter Muhongo na William Ngeleja, ambao pia walitajwa katika ripoti ya kamati ya makinikia ya Profesa Abdulkarim Mruma kuwa walihusika kwa njia moja au nyingine katika sakata la makinikia.

Wengine ni George Simbachawene, ambaye ni Waziri wa Tamisemi na Edwin Ngonyani (naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).

Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Madini mwaka 2015 baada ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kulazimika kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyoondoa mawaziri wawili, akiwamo Profesa Muhongo, ambaye aliwajibishwa kwa kutowajibika vyema kulinda mapato ya Serikali.

Jana, akisoma ripoti ya Kamati ya tanzanite iliyoundwa na wajumbe kumi na moja, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dotto Biteko alisema imebaini kuwa Tanzania haijawahi kunufaika na madini hayo. Alisema ni asilimia 20 pekee ya madini hubaki nchini huku asilimia 80 ikiwanufaisha wageni.

Biteko alisema Taifa limeingia hasara kubwa kutokana na ubia uliopo kati ya Shirika la Madini (Stamico) na kampuni ya Tanzanite One (TML) huku baadhi ya watendaji wakihusika kwa kupitisha usajili na mikataba kinyume cha sheria za madini.

Alisema mwaka 2015 Simbachawene akiwa wizarani hapo, aliridhia kuuzwa kwa hisa za kampuni ya Tanzanite One kwa kampuni ya Hong Kong ya Sky Associate Limited ambayo haijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) wala kuwa na hati safi za ulipaji kodi na kutofuata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna wa Madini pamoja na Kamati ya Bunge.

Kampuni hiyo ya Tanzanite One iliuza hisa za Dola 22.5 milioni kwa kampuni ya Sky Associate Limited ambayo baadhi ya wamiliki wake ni Watanzania.

Hatua hiyo ilisababisha kampuni ya Tanzanite One kukwepa kodi ya Sh 21.85 bilioni ambayo ilikuwa inadaiwa kwa wakati huo na haijalipwa hadi sasa.

“Kampuni ya Sky Associate Limited haina hati ya kufanya biashara, haitambuliki Brela ambayo ndiyo taasisi ya kuratibu usajili wa kampuni, TRA haiifahamu,” alisema na kuongeza;

“Matokeo ya kuuza hisa yanaipa nguvu kampuni ya Sky Associate Limited katika kampuni ya Tanzanite One, maridhiano hayo yasingefanikiwa bila ridhaa ya wizara ya madini, ridhaa iliyotolewa tarehe 30 Januari, aliyekuwa waziri George Simbachawene ina dosari kisheria na ukiukwaji wa kiutendaji wa Serikali,” alisema.

Mbali ya Simbachawene, alisema naibu waziri Ngonyani wakati huo akiwa kuwa kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, alitoa taarifa kwa umma juu ya maridhiano hayo ambayo yamedaiwa kusababisha hasara kwa kulinyima shirika hilo la umma nguvu ya uamuzi kwenye kampuni ya Tanzanite One waliyoingia ubia wa asilimia 50 kila mmoja kuendesha Mgodi wa Mererani.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa dosari katika utoaji wa leseni, maudhui ya mikataba na utekelezaji mbovu umesababisha hasara ya zaidi ya Sh157 bilioni na upotevu wa tani mbili za tanzanite kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi mwaka huu.

Pia, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepoteza Sh18 bilioni ambazo hazikulipwa na kampuni ya Tanzanite One kati ya mwaka 2009/17 huku ikikosa mgao wa faida zaidi ya Sh11.7 bilioni kutokana na kuingia mikataba mibovu iliyoikosesha nguvu Stamico.

Kamati ilieleza kuwa Ngeleja aliyekuwa waziri, aliacha kampuni hiyo kuendelea kuchimba madini pasipo na leseni kwa kipindi cha miaka mitatu (2010-2013) na kusababisha hasara ya Sh37 bilioni kutokana na ucheleweshwaji wa leseni.

Ilisema Profesa Muhongo alitoa leseni hiyo bila kupata ushauri wa Bodi na kutoa leseni zaidi ya 700 kwenye eneo la Mererani kinyume na taratibu.

Mapendekezo

Kamati hiyo imetoa mapendekezo mbalimbali kudhibiti biashara ya madini pamoja na kujenga kituo kimoja cha kuuzia madini (one stock centre) pamoja na kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya madini ili kuzuia utoroshaji.

Kamati imependekeza kuanzishwa kwa benki ya madini ili kuyahifadhi na kuuza pamoja na kupitia upya mikataba ya madini.

“Kamati inapendekeza kuwa kampuni zote za TML ikiwa na akaunti zake ndani na nje ya nchi ziwekwe chini ya ulinzi kwanza wakati Serikali inatafakari cha kufanya juu ya hicho kilichotokea,” alisema Biteko.

Mbowe anena

Akizungumzia ripoti hiyo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema kuundwa kwa kamati za madini kumeisaidia Serikali kubaini mambo makubwa ambayo yanahitaji hatua za haraka.

Alimuomba Spika wa Bunge kuruhusu matokeo hayo kujadiliwa bungeni ili kuja na mapendekezo ya pamoja jambo ambalo hata hivyo, Spika alisema itakuwa kurudi nyuma.

Waziri Mkuu

Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo na ile ya almasi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema zimetoa picha halisi juu ya ubadhirifu na upotevu wa madini na kuahidi kuchukua hatua stahiki kwa wote waliohusika.

“Serikali ina imani na kamati hizi. Kesho (leo) saa nne na nusu nitakwenda kumkabidhi mheshimiwa Rais ripoti hizi, hatuchelewi,” alisema.

Spika Ndugai aliwataka viongozi na wananchi kuwa wazalendo na uchungu na maliasili za Taifa.

Alisema ni lazima mifumo ipitiwe upya kwa kuwa imekuwa chanzo cha upotevu wa rasilimali nchini huku akishauri Wizara ya Nishati na Madini igawanywe kwa kuwa madini yamekuwa na mambo mengi.