Waziri Ndumbaro atia mguu kukamatwa kina Dk Slaa
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro
Muktasari:
- Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, amezitala taasisi za kimataifa kuacha kuingilia masuala yanayohusu nchi za Afrika ikiwamo kukamatwa kwa kina Dk Slaa, bali waviache vyombo vya dola vitekeleze wajibu wake.
Arusha. Siku chache baada ya kukamatwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi, Mpaluka Nyagali na Dk Wilbroad Slaa, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro, ameonya mashirika ya kimataifa likiwemo Amnesty International, akiyataka kuacha kuingilia mambo ya nchi za Afrika na badala yake waachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.
Kauli ya Dk Ndumbaro imetoka siku moja baada ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye naye kutoa tamko kwa mashirika hayo, akisema watuhumiwa hawakukamatwa kwa kukosoa mkataba wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai.
Shirika la utetezi wa haki za binadamu la Amnesty International lilitoa taarifa yake Agosti 14, 2023 liikitaka Serikali kuwaachilia wanaharakati hao kupitia tovuti yake.
Dk Slaa na wenzake wanashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kukamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Agosti 12 na 13, 2023.
Akizungumza katika kongamano la huduma ya msaada wa kisheria na upatikanaji haki kwa wananchi linalofanyika mkoani Arusha leo Alhamisi Agosti 17, Dk Ndumbaro amesema suala hilo limeshafikishwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Amesisitiza kuwa kukamatwa kwao hakuhusiani na ukosoaji wao katika mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA).
Ameitaka Amnesty International na taasisi nyingine za kimataifa kutambua kuwa inaongozwa na Katiba na Sheria, ambazo kuwa mhalifu anapokamatwa baada ya upelelezi atafikishwa mahakamani na mahakama ndiyo itaamua.
"Amnesty International siyo mahakama ya Tanzania, sisi tuna mahakama zetu na tutaendelea kuziheshimu, kwenye hili tuviache vyombo vya dola vifanye kazi yake.
“Kama wewe unaamini kwamba mtu wa kawaida hawezi kufanya na kupanga uhaini uje mahakamani utoe ushahidi ili wote tukusikie pale ukiongea chini ya kiapo na ukiulizwa maswali yale ya cross examination (maswali ya dodoso).
Huku akitoa mfano wa kesi tatu zinazomkabili Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump, Dk Ndumbaro amehoji,
“Tumewahi kuwasikia Amnesty International wanatoa kauli kwamba kwa sababu Trump anatoka upinzani, serikali ya Biden inakandamiza upinzani? Sasa tunawaomba Amnesty International watoe kauli zile kesi za Trump kule na sisi tuwasikie," ameongeza.
Dk Ndumbaro ametaja miongoni mwa waliokosoa mkataba huo ni pamoja na Prof Anna Tibaijuka ambapo alidai hata hivi karibuni alihojiwa na vyombo vya habari vya kimataifa akaendelea kukosoa pamoja na TLS ambao walitia waraka wao kukosoa lakini hawajakamatwa kwa kuwa hawajakiuka sheria yoyote.
Dk Ndumbaro amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani ibara ya 18 inatoa haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni miongoni mwa haki nyinginezo.
Kuhusu mawakili 100 wanaotarajiwa kuwatetea watuhumiwa hao watatu, Waziri Ndumbaro amesema kuna Watanzania wengi wako mahabusu na hawana mawakili, lakini anajiuliza kwa nini hawapigiwi kelele.
"Niwaombe na nimepata taarifa kuna mawakili zaidi ya 100 watakwenda kuwatetea hawa watu hiyo ndiyo njia sahihi, mawakili hao 100 wajipange waende mahakamani wakathibitishe ile siyo uhaini, ugaidi, kauli za kueneza chuki na wakifanikiwa kufanya hivyo mahakama ikikubalana nao ndiyo utawala wa sheria," amesema Dk Ndumbaro.
Kwa upande wake Rais wa TLS, Harold Sungusia, amesema walishawasilisha suala hilo mamlaka za juu na wameendelea kulifuatilia na kuwa chama hicho kinasimamia utawala wa sheria na endapo mtu ametuhumiwa afikishwe kwenye chombo cha haki na mahakama kuamua
"Tulishawasilisha hili suala kwa mamlaka za juu na tumeendelea kufuatilia kwa sababu anayeamua mtu amekosea au hajakosea ni mahakama kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo yanaendelea hapa kati," amesema Sungusia