Waziri Ummy aagiza elimu mipakani tahadhari ya Ebola

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa katika kata ya Kashenye wilaya ya Misenyi.
Muktasari:
- Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wataendelea kuchukua tahadhari kuhakikisha ugonjwa wa ebola hauingii nchini kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo waganga wa kienyeji.
Bukoba. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wataendelea kuchukua tahadhari kuhakikisha ugonjwa wa ebola hauingii nchini kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo waganga wa kienyeji.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 04, 2022 wakati akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera, ambapo amesema, watahakikisha wanatoa elimu kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji, watendaji wa kata na vijiji, madiwani pamoja na waganga wa kienyeji.
"Lazima tuchukue tahadhari kuhakikisha ugonjwa hauingii nchini, tuendeleze jitihada za kuzuia mipaka rasmi ni michache ni lazima tukatoe elimu kwa viongozi ngazi ya kata, vijiji, vitongoji, bodaboda na kwa waganga wa kienyeji makundi haya ndo yapo karibu na wananchi lazima tuyafikie" amesema Mwalimu
Mganga mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issessanda Kaniki awali akisoma taarifa ya afya amesema ili kudhibiti ebola mkoa huo unahitaji kutoa elimu zaidi kutokana na mkoa kuwa na mipaka 1200 inayoingia nchi jirani huku mipaka rasmi ikiwa saba.
Dk Kaniki amesema mkoa huo unahitaji magari tisa ya wagonjwa na kituo kikubwa cha matibabu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alimshukuru Waziri kwa kuleta maabara tembezi ya kupima virus vya ebola iliyofungwa kituo cha afya Kabyaire kilichopo wilaya ya Misenyi.
Chalamila amependekeza vituo vya kutolea huduma viwekwe wilaya ya Ngara ambayo ina mipaka miwili Rusumo kuingia Rwanda na Kabagara kuingia Burundi kituo kingine kijengwe Murongo wilaya ya Kyerwa ambao ni mpaka wa kuingia Uganda.
Aidha Waziri Ummy baada ya hapo ameendelea na ziara ya kukagua mipaka inayoingia nchi ya Uganda ambayo ni mpaka wa Kashenye ambao siyo rasmi na mpaka wa Mtukula ambao ni rasmi.