Prime
Wema wa kusaidia mzigo wa mtu unavyoweza kukuponza
Dar es Salaam. “Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo niliwahi kumsaidia mama mmoja aliyepanda kwenye daladala akiwa amechoka kumbeba mtoto aliyekuwa naye nikatumia hekima na utu wangu kutokana na uchovu wake, lakini kumbe bila kujua naenda kuangushiwa jumba bovu.
“Nilivyombeba mtoto huyo mwenye umri kati ya mwaka mmoja na nusu hadi miwili kuanzia kituo alichopanda katika Barabara ya Morogoro maeneo ya Manzese nikiwa na furaha ya kucheka na mtoto huyo huku safari ikiendelea, lakini jambo la ajabu wakati nataka kushuka mama huyo hakuonekana tena ndani ya daladala na mtoto niko naye mimi,” amesema mkazi wa Dar es Salaam, Hassan Abdallah.
Abdallah ni moja ya waathirika wa kutelekezewa mtoto aliyembeba kwa wema akidhani anatoa msaada kumbe ilikuwa mwanzo wa changamoto aliyokumbana nayo.
“Basi nikisaidiana na abiria wenzangu kushangaa na kutafuta mama huyo ameenda wapi huku mtoto akiwa analia ukaja ushauri ya kwamba nimeshatelekezewa cha msingi tukatoe taarifa kituo cha polisi kilicho karibu,” amesema.
Abdallah kwa kuwa ndiye aliyekuwa na mtoto kwa wakati huo ikabidi akubali kwenda kituo cha polisi na gari zima kutumika kama ushahidi kwa hilo lililotokea.
Baada ya kufika akitoa maelezo huku akisaidiwa na mashuhuda akapewa kuandikisha huku akimkabidhi mtoto huyo mikononi mwa polisi, huku akitakiwa kwenda kuripoti kila siku na kuangalia kama mama huyo amejitokeza kumfuata mtoto wake huyo.
“Kwa kweli jambo hili liliniachia doa tangu siku hiyo sikuwahi kushika kifurushi wala mzigo wa mtu kwenye gari (daladala) nilijifunza jambo kuwa wema wa mtu unaweza kumponza na mfano ni mimi mwenyewe,” amesema.
Simulizi ya Abdallah haiishii kwa mtoto pekee bali ni funzo kwa tabia ya kubeba mizigo, vifurushi au mabegi kutoka kwa mtu usiyemfahamu katika usafiri wa umma hasa katika majiji makubwa yenye watu wengi bila kujua ni nini kipo ndani kwani hatua hiyo inaweza kukusababishia matatizo makubwa.
Msingi wa habari hii unatokana na onyo la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kuwa kitendo cha kumsaidia kubeba mtu kifurushi/mzigo kinaweza kuwa mwanzo wa matatizo ya kisheria kwa muhusika hasa pale itakapobainika ni dawa za kulevya.
DCEA inasema wapo watu wenye nia mbaya ya kuwatumia abiria na watu wasio na hatia kusafirisha dawa bila ya wao kufahamu hivyo ni heri kuepuka kufanya wema wa namna hiyo.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Dar es Salaam, Esther Daud anasema binafsi yeye hana tabia ya kumsaidia mtu mzigo hata wakiwa kwenye daladala kwakuwa hajui nini kimo ndani na endapo mtu huyo akimuachia.
“Kama mtu amekupatia furushi la madawa au vitu vinavyoweza kukupeleka jela utajuaje? mimi sina hiyo tabia acha nionekane nina roho mbaya kwa kweli,” amesema.
Alichokisema Esther kinamfungua Amina Ramadhan anayesema ana tabia hiyo ya kuonea watu huruma na kuwabebea mizigo yao hata akiwa katika safari za kila siku za daladala zenye watu wengi ndani.
“Unaweza ukamsaidia kwa wema kwakuwa unamuona amechoka au ameshindwa kusimamia vizuri na baadaye akiwa anashuka akakukabidhi mzigo wake, maisha yakaendelea na nimeshawafanyia hivyo wengi,” amesema.
Amina yeye anasema haoni kama kuna kosa kufanya wema wa namna hiyo ingawa watu wengi sasa hivi sio wa kuwaamini.
Ikumbukwe kwa wengi, kitendo hicho ni ishara ya utu, upendo na mshikamano wa kijamii. Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya usalama wanaonya kuwa wema huo usio na tahadhari unaweza kugeuka chanzo cha matatizo makubwa ya kuhusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya au bidhaa nyingine haramu bila muhusika kujua.
Katika vituo vya mabasi na maeneo yenye msongamano wa watu, baadhi ya wahalifu hutumia ujanja wa kuwaomba wasafiri wawabebee mizigo wakidai wanaelekea eneo moja au watachelewa kuingia kwenye gari. Mara nyingi mizigo hiyo hukabidhiwa bila mwenye kubeba kujua kilichomo ndani.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Polisi nchini, Jamal Rwambow amesema sio busara hata kidogo kubeba mzigo wa mtu hujui kuna nini na siku zote wahalifu wamekuwa na mbinu nyingi ya kutumia ukarimu wa Watanzania kuwabebea mizigo yao.
“Ukikamatwa na hiyo mizigo wewe ndiyo utawajibika kwa kuwa umekutwa nalo wewe wote mnaunganishwa, kinachohitajika ni umakini wa hali ya juu,” amesisitiza Rwambow.
Jenista Antony amesema amewahi kuombwa kubeba mfuko na mtu asiyemfahamu kwenye daladala akidai anakwenda kushuka kituo kinachofuata.
“Wakati huo niliona ni jambo la kawaida, lakini baada ya kusikia matukio ya watu kukamatwa na mizigo yenye vitu haramu niligundua kuwa nilikuwa nimejiweka kwenye hatari kubwa,” amesema.
Ikumbukwe hata, Jeshi la Polisi limekuwa likitoa tahadhari mara kwa mara kwa wananchi kuepuka kubeba mizigo ya watu wasiowafahamu bila kujiridhisha kuhusu mmiliki na yaliyomo ndani ya mzigo husika.
Mbali na dawa za kulevya, wahalifu wanaweza kutumia njia hiyo kusafirisha bidhaa za magendo, fedha zinazohusishwa na uhalifu, nyaraka bandia au vitu vilivyoibwa.
Suluhisho
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Wakili Aloyce Komba amesema tabia hiyo ni hatari na kisheria utakayekutwa na mzigo huo una kesi ya kujibu kwa kuwa kutokujua sheria siyo utetezi, huku akisema kwenye kesi ya namna hiyo sheria inasema kuna umiliki na usafirishaji.
Anasema anaweza akawa mtu unayemfahamu au hata usiye mfahamu akuombe umsafirishie mzigo huku akisema cha kufanya umuulize huo mzigo ni wa nini na kama utaweza ukague kujiridhisha ili kujiepusha na matatizo.
“Watanzania tuwe na tahadhari tujue tusiwe na upendo wa namna hiyo tusije kujiingiza kwenye matatizo kwa maana uhalifu upo kila mahali, unaweza ukakabidhiwa mtoto kumbe mtoto huyo kaibwa,” ameshauri.