Wenye ualbino waomba mafuta yao

Muktasari:
- Chama cha watu wenye ualbino nchini (TAS) Mkoa wa Mwanza kimeiomba serikali kurahisisha upatikanaji wa mafuta ya kukinga ngozi yao dhidi ya mionzi ya jua kuwaepusha na ugonjwa wa saratani yaweze kupatikana hadi hospitali za wilaya na maeneo ya vijijini.
Mwanza. Chama cha watu wenye ualbino nchini (TAS) Mkoa wa Mwanza kimeiomba serikali kurahisisha upatikanaji wa mafuta ya kukinga ngozi yao dhidi ya mionzi ya jua kuwaepusha na ugonjwa wa saratani yaweze kupatikana hadi hospitali za wilaya na maeneo ya vijijini.
Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Stalone Makoye amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hizo na kufanya kundi hilo lishindwe kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi na ujenzi wa taifa ambazo zinafanyika wakati wa jua kali.
Ametoa ombi hilo leo jijini Mwanza katika kikao cha kamati ya amani ya mkoa huo na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa tamko la viongozi wa dini kuhusu haki na ustawi wa watu wenye ualbino nchini ambapo amesema mafuta hayo yanauzwa kuanzia Sh 50,000 hadi 70,000 kwa kopo moja ambalo linaweza kutumika kwa miezi mitatu na mtumiaji anapaswa kupaka mara tatu kwa siku moja.
“Watu wenye ualbino wanaweza kushiriki kulijenga taifa kwa kushiriki shughuli za maendeleo kwahiyo tunaomba tuwezeshwe mafuta haya kuimarisha afya zetu kwani kwa sasa kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wake wilaya nyingi hazina mafuta hayo hivyo kufanya iwe ngumu kushiriki shughuli za kiuchumi kujiingizia kipato,” amesema Makoye.
Mmoja wa akina mama wenye ualbino, Monica Yusuph amesema mbali na changamoto hiyo wanawake wenye ualbino wanapata shida ya kupata wenza na kuolewa kutokana na wasiwasi walionao na watu wanaowafuata kuwahitaji huku akifichua kuwa baadhi ya wanajamii wameanzisha dhana potofu kuwa ukishiriki mapenzi na mwanamke mwenye ualbino unapona maradhi ya Ukimwi na kuitaka serikali kutoa elimu kuondoa dhana hiyo.
Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa Serikli, taasisi za dini, watu wenye ualbino na wanajamii kila mmoja wanapaswa kutimiza wajibu wao katika kushawishi mabadiliko chanya ya kifikra kwenye jamii juu ya haki na utu wa watu wenye ualbino nchini ili kuondoa unyanyapaa, mauaji na kukatwa viungo.
Ameiomba serikali kuboresha na kusimamia sharia zinazolinda kundi hilo, kutengeneza na kusimamia sera rafiki zitakazowapa vipaumbele, kutoa mrejesho ya maendeleo ya watu wenye ualbino na kupitisha rasimu ya mwongozo wa utoaji huduma za elimu kwa kundi hilo nchini na kuhamasisha wahudumu wa afya kuzingatia miongozo ya matibabu kwa kundi hilo.
“Tunatambua uwepo wa vitendo vya unyanyapaa kwa watu wenye ualbino ndiyo maana tunasisitiza elimu kwa jamii ambayo bado inahitajika kwa kiasi kikubwa, sisi viongozi wa dini tunaamini katika waumini wote wa dini kuheshimu uhai wa binadamu na kukemea aina zote za unyanyapaa dhidi ya watu hawa,” amesema Askofu Sekelwa.