Wenye ulemavu walalamikia unyanyapaa

Baadhi ya wanawake wenye ulemavu wakiwa katika mafunzo  yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Movement for Women with Disability Tanzania-MOWADITA kwa udhamini wa  UN-Women  pamoja na ADD International. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Wanawake wenye ulemavu wasimulia namna wanavyokutana na unyanyapaa katika chaguzi mbalimbali, hasa wanaposimama na kutaka kugombea nafasi za uongozi.

Mtwara. Licha ya wanawake wenye ulemavu kukumbana na changamoto za unyanyapaa katika jamii, wametakiwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu.

Hamasa hiyo imetolewa leo Aprili 23, 2024 na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Movement for Women with Disability Tanzania (Mowadita), Nuru Awadh kwenye mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika mkoani Mtwara yakidhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) pamoja na ADD International.

Amesema kumekuwa na mitazamo ya aina tofauti kuhusu wanawake wenye ulemavu, hivyo kuhisi kunyanyapaliwa ni hali ambayo inawarudisha nyuma na kushindwa kutimiza haki zao za kikatiba za kupiga na kupigiwa kura.

“Wakati mwingine wanashindwa kuaminika kwa sababu ya mtazamo, hata ukitaka kugombea wanaanza kusema ataweza vipi wakati haoni, huo ni mtazamo wakati sheria inamruhusu mtu mwenye ulemavu kupiga  na kupigiwa kura.”

“Zipo hali ngumu wanazopitia watu wenye ulemavu, tunataka wajue haki zao na wajibu, ndio maana tunawapa elimu wajitambue ili wazifikie na kuzipambania fursa za kiuchumi,” amesema Awadhi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Mowadita, Dorice Kulanga amesema lengo la kuwajengea uwezo walemavu ni kuwawezesha, kuwafundisha utawala bora na uchumi ili wajue haki zao za kiuchumi.

“Wanawake wengi wenye ulemavu wameachwa, tunataka kuwapa misingi ya utawala bora na kuzijua fursa za kiuchumi wapi waende wafanye nini ili waweze kuwa sehemu ya kuchangia pato la Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Fatuma Mpondomoka, mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wenye Ulemavu Manispaa Mtwara Mikindani, amesema mara kadhaa wamekuwa wakinyanyapaliwa na kushindwa kutembea mtaani hasa siku za Alhamisi na Ijumaa.

“Unaweza kuamua kutembea hasa Alhamisi na Ijumaa unadhihakiwa wakidhani ni ombaomba wapo ambao wanadiriki kujificha wakituona, yaani ukishakuwa mlemavu wanahisi kuwa ndio umechoka kabisa kimaisha.”

“Sio sawa kwamba kila mlemavu ni ombaomba, wengine wanatuongelea vibaya, ukiwa mlemavu sio kwamba akili nayo imelemaa, watuamini ili tuweze kufanya kazi zetu kwa uhuru,” amesema.

Naye, Zamda Abdallah, mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wenye Ulemavu Mkoa wa Mtwara amesema kuwa unyanyapaa umekuwa ukiwaumiza kwa kiasi kubwa, hivyo kuwafanya washindwe kusimama na kugombea.

“Wakati mwingine tunaposimama kugombea watu wanatukashifu na kutuita vilema hiyo inatufanya tusiwe na ujasiri, yaani tumekuwa na shida lakini sasa nimepata ujasiri nitasimama na kugombea,” amesema.