Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye vyeti feki wakaangwa bungeni

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Ni baadhi ya mawaziri, wabunge wanaotajwa, wataka wathibitishe uhalali wake.

Dodoma. Wabunge juzi jioni walichachamaa wakitaka mawaziri na wabunge wanaohusishwa na vyeti feki kulithibitishia Bunge juu ya uhalali wa vyeti vyao.

Suala hilo lilijitokeza wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/15.

Wabunge hao walikuwa wakijadili hoja iliyotolewa na Mbunge wa Ole, Rajabu Mohamed Mbarouk (Cuf) aliyeitaka Serikali kueleza ni kwa nini Baraza la Mitihani ya Taifa (Necta) linashindwa kudhibiti vyeti feki. Alisema kuna mchezo mchafu unaoathiri mfumo wa elimu nchini na uchumi wa Taifa.

Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunaifanya hadhi ya Necta kushuka na kukosa imani hata katika jumuiya za kimataifa.

“Suala la vyeti feki ambalo Baraza la Mitihani la Taifa ndilo lenye dhamana na jukumu la kuhakikisha halitokei katika taifa limeonekana kama suala la kawaida,” alisema na kuongeza; “Vyeti feki ni vingi kiasi kwamba linasababisha kuajiriwa kwa watendaji ambao ni feki na mawaziri mizigo.”

Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunasababisha kupata makatibu wakuu na watendaji feki.

Mbarouk alisema hivi karibuni katika Chuo cha Polisi cha Moshi walirejeshwa wadahiliwa 122 kwa sababu ya kukutwa na vyeti feki.

Alihoji ni kwa nini Necta inashindwa kudhibiti vyeti hivyo.

Akitoa ufafanuzi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema Necta baada ya kugundua udanganyifu wa vyeti ilibadilisha namna ya kuchapa vyeti hivyo.

“Hivi sasa vyeti vinavyotolewa vina Serial number, jina la mhitimu katika cheti cha kuzaliwa na picha na kwamba siyo rahisi kughushi vyeti hivyo,” alisema.

Hata hivyo, Mbarouk alikataa ufafanuzi huo na kusema asilimia sita ya wanaoomba kazi nchini wana vyeti feki.

Alitaka kufahamu hatua zilizochukuliwa ikiwamo za kinidhamu katika kukabiliana na suala hilo.

Hoja hiyo iliungwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (Cuf) aliyesema suala la kuweka namba, picha lilianza kufanyika tangu mwaka 2012 lakini bado tatizo liko.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) aliunga mkono hoja hiyo na kusema kitabu cha Msemakweli katika toleo la pili la dharura alieleza kuwa kuna wabunge, mawaziri na madokta feki.

Alisema jambo hilo linaweka ugumu kwa Serikali kulisimamia suala hilo nje ya Bunge.

“Hawa watu tuko nao humu ndani hawajakanusha, ndiyo maana tuna mawaziri mizigo kwa sababu wana vyeti feki. Serikali isiwe na kigugumizi hawa watu waonekane hapa hadharani,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR-Mageuzi) alisema msako wa kuwasaka walio na vyeti feki ungeanzia bungeni.

“Kama inafika wakati watu wanataja ni mawaziri na wabunge wana vyeti feki halafu Bunge lako bado linakaa kimya tutegemee watu wataenda kupiga dili huko la vyeti feki,” alisema Machali.

Aliwataka mawaziri na wabunge wanaotajwa kuwa na vyeti feki kutajwa bungeni na kisha wathibitishe.

Alisema vinginevyo wabunge hao wasipotajwa ndani ya Bunge wategemee kuwa suala la vyeti feki litaendelea.

“Wale wanaotajwa watuambie kama kweli wana digrii feki au la,” alisema Machali.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais, (Utumishi), Celina Kombani alisema Serikali inafanya juhudi kuzuia watu wanaoajiriwa wasiwe na vyeti feki.

“Kama mtu ana cheti feki, mfumo unakataa. Vyeti feki vinatengenezwa mitaani havitengenezwi na Baraza la Mitihani,” alisema na kuongeza;

“Na nyie msinyooshee vidole wenzenu na nyie mpo humu ndani.”

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema Necta imekuwa ikidhibiti vyeti feki visiingie serikalini.

“Baadhi yetu si ajabu mnatengeneza vyeti feki. Hata wabunge wapo. Na kambi ya Chadema mnaye mbunge ambaye ana cheti feki cha kidato cha nne,” alisema na kuongeza;

“Tunamjua (akakatizwa na kelele za wabunge waliomtaka kumtaja), mwenyewe anajifahamu.”

Alisema mbunge huyo hajafika kidato cha nne lakini ana cheti cha kidato cha nne.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati ya matumizi, Job Ndugai alisema suala la vyeti feki si la Tanzania peke yake kwa kuwa lipo hata katika nchi jirani za Kenya na Uganda na mahali pengine.

Alipoulizwa kuhusu wabunge wanaotuhumiwa kuwa na vyeti feki, Ghasia alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa sababu lilikuwa ndani ya Bunge.

“Hayo ni mambo yamezungumziwa ndani ya Bunge siwezi kuyazungumzia. Na si umesikia kuwa suala hilo limepelekwa katika Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge,”alisema Ghasia.