Wilaya ya Bukombe yalia upungufu wa wauguzi

Mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko (wa tatu kushoto) akifurahia jambo baada ya kupokea risala kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waunguzi Tanzania (TANNA) Wilaya ya Bukombe, Lucianus Ng'ella (kulia). Picha na Ernest Magashi.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Waunguzi Tanzania (TANNA) Wilaya ya Bukombe, Lucianus Ng'ella amesema wauguzi 203 kati ya wauguzi 263 waliopo wilayani humo wanafanya kazi katika vituo vya huduma vya umma huku 60 waliosalia wanafanyakazi katika vituo vya huduma vinavyomilikiwa na taasisi na watu binafsi vikiwemo taasisi za kidini.

Bukombe. Wilaya ya Bukombe inakabikiwa na upungufu wa wauguzi 158 katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za Serikali na watu binafsi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani, Muuguzi Mkuu Wilaya ya Bukombe, Diana Sahan amesema wilaya hiyo inahitaji wauguzi 421, lakini waliopo sasa ni 263 pekee.

Mwenyekiti wa Chama cha Waunguzi Tanzania (TANNA) Wilaya ya Bukombe, Lucianus Ng'ella amesema wauguzi 203 kati ya wauguzi 263 waliopo wilayani humo wanafanya kazi katika vituo vya huduma vya umma huku 60 waliosalia wanafanyakazi katika vituo vya huduma vinavyomilikiwa na taasisi na watu binafsi vikiwemo taasisi za kidini.

"Upungufu wa wauguzi kwenye vituo vyetu vya huduma za afya ni kero kwa wananchi kwa sababu wakati mwingine wanalazimika kusubiri huduma kwa muda mrefu. Tunaiomba Serikali iendelee kutoa fursa za ajira katika kada ya afya kukidhi kasi ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali,’’ amesema Ng'ella.

Mganga Mkuu Wwilaya ya Bukombe, Dk Deograsia Mkapa ameunga mkono ombi la Serikali kuongeza ajira za wauguzi kutokana na ukweli kwamba asilimia 80 ya wagonjwa wanaofika katika vituo vya huduma wanahudumia na kada hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amesisitiza ahadi ya Serikali ya kuendelea kutoa fursa za ajira za watumishi wa kada ya afya kadri hali na uwezo wa kiuchumi unavyoruhusu.

Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewaomba wauguzi nchini kuwa wavumilivu wakati Serikali inafanyia kazi changamoto zinazoikabili kada hiyo ikiwemo malipo ya Sh120, 000 sare kwa kila muuguzi kila mwaka.

Kuhusu idadi ya watumishi kulinganisha na vituo vya huduma, Biteko ambaye pia ni mbunge wa Bukomba ametaja muitikio na kasi ya wananchi ya kujenga miundombinu ya huduma za afya kuwa miongoni mwa sababu za upungufu huo huku akiahidi kuwa Serikali itaendela kuajiri watumishi kadri ya mahitaji na hali ya kiuchumi.

"Mwaka 2015 wilaya ya Bukombe tulikuwa na zahanati mbili, vituo vya afya viwili na hospitali; lakini leo hii, Serikali kwa kushirikiana na wananchi imejenga zahanati 16, vituo sita vya afya, hospitali ya wilaya huku kituo kikipandishwa hadhi kuwa hospitali. Ni dhahiri tutahitaji watumishi zaidi,’’ amesema Dk Biteko

Amesema wilaya hiyo inaendelea na ujenzi wa zahanati nyingine mpya 20 wa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi huku akiwaomba wadau wa sekta ya afya kuendelea kuwekeza kwenye eneo hilo bila kusahau sekta zingine ikiwemo elimu, biashara na huduma.