Wizara ya Afya yazungumzia watoto wenye uzito uliopitiliza

Vumilia katikati akiwa na watoto wake Imani (6) ana uzito wa zaidi ya kilo 70 na mdogo wake Gloria (4) akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 50. Picha na Rachel Chibwete
Muktasari:
- Watoto hao ni Imani Joseph mwenye umri wa miaka sita ambaye ana uzito wa zaidi ya kilo 70 na Gloria Joseph (4) mwenye uzito wa zaidi ya kilo 50.
Dodoma. Wizara ya Afya imeeleza utaratibu unaotakiwa kufuatwa kwa wazazi wa watoto wenye uzito uliopitiliza ili waweze kupata kibali cha msamaha wa matibabu kwa changamoto inayowakabili.
Maelekezo hayo yametolewa siku moja baada ya tovuti hii kuchapisha habari inayohusu watoto Imani na Gloria wakazi wa Kata ya Makole jijini Dodoma, wenye uzito mkubwa kuliko umri wao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Januari 14, 2024, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo amesema wazazi wa watoto hao wanatakiwa kuanza taratibu za matibabu kuanzia ofisi za serikali ya mtaa wanapotoka ambako watapewa barua.
Amesema barua hiyo inatakiwa iwatambulishe kuwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya watoto wao ambayo itaenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mkurugenzi huyo amesema barua hiyo ya utambulisho itawasaidia kufuata utaratibu wa rufaa hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, badala ya kwenda huko moja kwa moja.
"Wakisema waanzie moja kwa moja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili watatumia gharama kubwa kwa sababu wataonekana ni private (wanajilipia), hivyo ni lazima waanzie ngazi za chini ili wafike huko kwa njia ya rufaa ili wasaidiwe," amesema Profesa Rugajjo.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Hospitali ya Muhimbili –Mloganzila, Dk Erick Muhumba amesema matibabu ya watoto hao yanawezekana, kinachotakiwa ni kufikishwa hospitalini na kuanzishiwa vipimo ili kujua tatizo ni nini ili waanzishiwe matibabu.
Watoto hao ni Imani Joseph mwenye umri wa miaka sita ambaye ana uzito wa zaidi ya kilo 70 na Gloria Joseph (4) mwenye uzito wa zaidi ya kilo 50.
Wazazi wao Joseph Kalenga na Vumilia Elisha, wameomba msaada wa matibabu ya watoto wao ili wawe na uzito wa kawaida sawa na wengine wenye umri sawa na wa kwao.
Dk Muhumba amesema tatizo walilonalo linaweza kuwa ni homoni kuzidi au kupungua au aina ya vyakula wanavyokula, hivyo wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wajue sababu ni nini ili waanzishiwe matibabu.
Amesema kama tatizo ni homoni kama walivyoambiwa mwanzo yapo matibabu ya vidonge vya kuongeza au kupunguza, ambavyo watatumia na hali zao zitakaa sawa.
"Kuhusu kufanyiwa operesheni ya kuwekewa puto tumboni, hilo haliwezekani kutokana na umri walionao bado ni mdogo lakini kuna vidonge vya kutumia ambavyo gharama yake si kubwa na hali zao zitakaa sawa," amesema Dk Muhumba.
Akizungumzia lishe kwa watoto hao, ofisa lishe kutoka Wizara ya Afya, Japheth Msoga amesema pamoja na lishe kuchangia uzito wa mtoto lakini hali ni tofauti kwa wawili hao ambao wameanza kuongezeka uzito hata kabla ya kuanza kula vyakula vingine nje ya maziwa ya mama.
Amesema hapo suala la homoni linachangia zaidi kuongezeka uzito kwani hata kama wanakula sana, lakini wanatumia vyakula ambavyo vinaliwa na watu wote bila kuwaletea madhara ya uzito kupitiliza.
Msoga amesema suala la kuwapatia mlo kamili wenye mboga nyingi, maji na matunda linaweza kupunguza ongezeko la uzito kama hakuna sababu nyingine yoyote inayochangia kuongezeka kwao.
Amesema Wizara ya Afya itafika na kuwaona watoto hao ili wajue namna bora ya kuwasaidia kwani si kawaida kwa watoto kuongezeka uzito kwa kasi hiyo.
Familia hiyo ina watoto wanne, huku Imani na Gloria wakiwa na uzito mkubwa kuliko umri wao, hivyo kutishia usalama wa afya yao.
Baba mzazi wa watoto hao, Kalenga alisema wanawe wanakula chakula kingi kuliko kawaida kwa kuwa wakitengewa kilo tano za wali au ugali wanamaliza.
Kalenga alisema analazimika kutumia Sh30,000 kila siku kwa ajili ya chakula kutokana na watoto hao kula chakula kingi.
Kutokana na uzito huo, watoto hao wanashindwa kucheza na kujumuika na wenzao.
Vumilia alisema watoto wake wanapenda kujichanganya na wenzao kwenye michezo, lakini huishia kuwa watazamaji tu kwa kuwa wanashindwa kuendana na kasi ya wenzao.
Kalenga ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuwasaidia watoto wake kupungua uzito ili iwe rahisi hata kuanza shule.