Wazazi wenye watoto waliopitiliza uzito waiangukia Serikali

Vumilia katikati akiwa na watoto wake  Imani (6)  ana uzito wa zaidi ya kilo 70 na mdogo wake Gloria (4) akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 50. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Mama wa watoto hao, Vumilia amesema mpaka sasa Imani (6) ana uzito wa zaidi ya kilo 70 huku mdogo wake Gloria (4) akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 50.

Dodoma. Wakati furaha ya kila mzazi ni kuona mtoto wake akiwa na uzito unaoridhisha aghalabu akiwa kibonge kiasi cha baadhi ya wazazi kuwalisha vyakula vya aina mbalimbali kila mara. Hali ni tofauti kwa familia ya Joseph Kalenga na mkewe Vumilia Elisha wa mtaa wa Makole, Kata ya Makole jijini hapa, baada ya watoto wao kuongezeka uzito kupita kiasi.

Familia hiyo yenye watoto wanne, wawili kati yao Imani Joseph (6) na Gloria Joseph (4) wana uzito kuliko umri walionao,  hivyo kutishia usalama wa afya zao.

Kwa mujibu wa Kalenga, watoto hao wanakula chakula kingi kuliko watoto wenye umri kama wao.

“Wana uwezo wa kula na kumaliza  kilo tano za wali au ugali.

Wakizungumza na Mwananchi Digital katika mahojiano maalumu, wazazi wa watoto hao wanasema kuwa uzito unawafanya washindwe kucheza na kufanya mambo ambayo wenzao wanafanya kama sehemu ya maisha ikiwemo michezo.

Mama wa watoto hao, Vumilia amesema mpaka sasa Imani (6) ana uzito wa zaidi ya kilo 70 huku mdogo wake Gloria (4) akiwa na uzito wa zaidi ya kilo 50.

Uzito huo kwa mujibu wa Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige, “Mtoto mwenye umri wa miaka minne anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 16 na mwenye umri wa miaka sita anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 22 hii haijalishi anaishi Ulaya au Tanzania hii ndiyo kanuni afya.

Amefafanua uzito wa mtoto hupimwa kwa kuchukua umri wake ukazidisha mara mbili ukajumlisha na nane (4x2+8= 16).

Hata hivyo, Vumilia ameelezea historia ya watoto hao akisema walizaliwa wakiwa na uzito wa kilo 3 lakini walikuwa wanaongezeka uzito ka kasi kila mwezi, kati ya kilo tatu hadi nne hali iliyowashtua hata wataalamu wa afya kliniki ambao walimshauri kuwanyonyesha kwa ratiba maalumu.

Vumilia amesema Imani alizaliwa na kilo tatu na baada ya kumaliza mwezi mmoja alipopimwa kliniki alikutwa na kilo saba, hali ambayo haikuwashtua wengi.

Lakini alipofikisha miezi miwili alikutwa na kilo 10 ndipo manesi walimshauri awe anamnyonyesha kwa ratiba ili asiongezeke uzito kwa kasi, jambo ambalo amesema halikusaidia kitu.

Amesema pamoja na kumnyonyesha kwa ratiba kama alivyoshauriwa na wataalamu lakini alipofikisha miezi mitatu alikutwa na uzito wa kilo 15, hivyo alishauriwa aende hospitalini kwa ajili ya vipimo zaidi.

“Kwa wakati huo alikuwa hatumii chakula chochote zaidi ya kunyonya tu maziwa lakini uzito wake ulikuwa unaongezeka kwa kasi,” amesema Vumilia.

Amesema alipoona mtoto anaongezeka uzito kwa kasi waliamua kumpeleka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya vipimo, lengo kuona kama ana tatizo lolote la kiafya lakini vipimo vilionyesha hakuwa na tatizo.

“Alipimwa ubongo, moyo, figo na viungo vyote vya mwili kuona kama ana shida yoyote ikiwemo ulemavu au magonjwa, lakini majibu yalionyesha kuwa hakuwa na tatizo lolote la kiafya zaidi ya uzito mkubwa, lakini walibaini ana tatizo la homoni,” amesema Vumilia.

Amesema pamoja na majibu hayo hakuridhika alikwenda kwenye hospitali nyingine kufanya vipimo ili kuona tatizo ni nini na majibu yalikuwa ni hayohayo kuwa wana tatizo la uwiano wa homoni,  na dawa yake ni kula kwa mpangilio ‘diet’ ili kupunguza uzito wake vinginevyo hana tatizo lolote.

Vumilia amesema baada ya kupewa majibu hayo alianza kumpa mlo wa kumfanya apungue mwili ambapo alifanikiwa kwa muda kidogo, lakini kutokana na ugumu wa maisha alishindwa kufuata ratiba na kuanza kumpa chochote kilichokuwa kinapatikana.

Amesema baada ya kuacha kumpa mlo kamili uzito wake uliongezeka maradufu kwani mpaka anafikisha miezi kumi alikuwa na uzito wa kilo 35, hivyo alimkatisha kwenda kliniki kutokana na kushindwa kumbeba.

“Tangu wakati huo mpaka sasa mtoto huyo amekuwa akiongezeka uzito na mpaka anafikisha umri wa miaka sita ana kilogramu 70,”amesema.

Kwa upande wa Gloria, Vumilia amesema alizaliwa na mwili mdogo japo alikuwa na uzito wa kilo 3, hivyo alimshukuru Mungu kwa kumpa mtoto mwenye afya njema, akitarajia kuwa na uzito wa kawaida kama watoto wengine.

Amesema naye alianza kuongezeka uzito kwa kasi kama kaka yake kwani mwezi wa kwanza kwenda kliniki alikuwa na kilo saba na aliendelea kuongezeka kila mwezi hadi alipofikisha umri wa mwaka mmoja na uzito wa kilo 25, hivyo alishindwa kumbeba kwenda naye kliniki tena.

Vumilia amesema huyo wa kike hajawahi kumpeleka hospitalini kumfanyia vipimo vyovyote kwani alichukulia uzoefu wa kaka yake na kuanza kumpa mlo kamili ili asiongezeke uzito, lakini kutokana na hali ngumu ya maisha amejikuta akiishia njiani na mpaka sasa ana uzito wa zaidi ya kilo 50.

Mama huyo amewaomba wataalamu wa masuala ya afya ya watoto kumsaidia ili wawe kama watoto wengine na waweze kusoma, kucheza kwa uhuru.

“Nilisikia kuna huduma inatolewa na Hospitali ya Mloganzila ya kupunguza uzito kwa kuwekewa puto tumboni, nawaomba wasamaria wema kunisaidia ili watoto wangu wafanyiwe huduma hiyo, ili uzito wao upungue,” amesema.

Amesema watoto wake wanapenda kujichanganya na wenzao kwenye michezo lakini mwisho wa siku wanaishia kuwa watazamaji tuu, kwani wanashindwa kuendana na kasi ya wenzao.

“Ukiwaomba wana hamu ya kucheza mpira na michezo mingine ya kitoto lakini wanashindwa kujichanganya, unawakuta wapo pembeni wakiangalia wenzao wanavyocheza,” amesema Vumilia.

Amesema furaha yake kama mama ni kuwaona watoto wake wakikua na kuchanganyika na wenzao kama ilivyo kwa watoto wenye umri kama wao.

Baba wa watoto hao, Joseph Kalenga amesema analazimika kutumia 30,000 kila siku kwa ajili ya chakula kutokana na watoto hao kula kingi.

Kalenga amesema Imani na Gloria wanaweza kutumia hata kilo tano za chakula kwa siku peke yao, hivyo kumfanya afanye kazi kwa bidii kwa ajili ya kuhudumia familia.

Amesema kazi anayoifanya ni ya machinga ya kuuza mitumba na mkewe anafanya biashara ya kuuza samaki, hivyo kipato chao hakiwatoshelezi kuhudumia familia ipasavyo kutokana na watoto wao wawili kula chakula kingi.

Kalenga ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuwasaidia watoto wake kupungua uzito ili iwe rahisi hata kuanza shule kwa sababu kwa uzito walionao hawawezi kutembea umbali mrefu.

Akizungumzia changamoto ya watoto kuwa na uzito uliopitiliza Daktari Bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Julieth Kabengula amesema kunasababishwa na vitu vingi siyo suala la homoni peke yake.

Dk Kabengula amesema watoto hao wanahitaji uchunguzi zaidi wa tatizo walilonalo kwa sababu kuwakadiria mlo peke yake hakuwezi kupunguza tatizo walilonalo.

“Ni lazima watakuwa na tatizo lingine linalosababisha kuongezeka uzito kwa haraka hivyo, wanatakiwa kuchunguzwa na madaktari bingwa wa watoto Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo kama wana bima ya afya waende kwa wataalamu,  wanaweza kuwa kama watoto wengine,” amesema Dk Kabengula.

Amesema kama tatizo ni homoni linaweza kurekebishika iwe ni kwa kuongeza au kupunguza, lakini pia linaweza kuwa limeleta na matatizo mengine ya kiafya ambayo yanahitaji uchunguzi wa kitaalamu zaidi.

“Pia wanahitaji kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuwaweka vizuri maana kwa umri walionao na uzito wao kama hawatachangamana na watoto wenzao na kufanya mazoezi, inaweza kuwaletea matatizo mengine ya kiafya,” amesema Dk Kabengula.