World Vision yatoa msaada tani 117 za chakula

Mkurugenzi wa shirika la world vision Tanzani, Gilbert Kamanga(Mwenye kofia) akikabidhi chakula kwa wanafunzi wa shule ya msingi Ketumbeine iliyopo wilayani Longido

Muktasari:

  •  Shirika la World Vision Tanzania leo Ijumaa Juni 24, 2022 limetoa msaada wa tani 117 za chakula cha wanafunzi katika shuleni zilizopo kata ya Ketumbeine wilayani Longindo.


Longido. Shirika la World Vision Tanzania leo Ijumaa Juni 24, 2022 limetoa msaada wa tani 117 za chakula cha wanafunzi katika shuleni zilizopo kata ya Ketumbeine wilayani Longindo.

Tani hizo zenye thamani ya Sh 227.3 milioni ni pamoja na mahindi tani 117, maharage tani 37 pamoja na mafuta ya kula 308 zenye ujazo wa lita 20.

Akikabidhi chakula hicho leo katika shule ya msingi Ketumbeine yenye wanafunzi 1414 ambayo ni moja ya shule 24 zinazonufaika na mradi wa Ketumbeine AP, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo nchini Tanzania, Gilbert Kamanga amesema jumla ya wanufaika wa chakula ni wanafunzi 10,272 kutoka Tarafa hiyo.

Aidha Kamanga ameitaka jamii ya wafugaji ya Kimasai kuanzisha mikakati ya upatikanaji wa chakula shuleni ili kuboresha afya ya wanafunzi pamoja na kuongeza ufaulu wa masomo kwa wanafunzi pale mradi utakapoisha.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ketumbeine, Felix Mungaya amesema kupitia mradi huo wa Ketumbeine AP kupitia shirika hilo ugawaji wa chakula shuleni umeleta matokeo chanya kwa wanafunzi kwa kupunguza utoro kwa baadhi yao kutokana na njaa.

Mmoja wa mnufaika wa mradi huo kutoka shule ya msingi Ketumbeine, Kaleb Israel (14) amesema wanalishukuru shirika hilo kuwapatia chakula kwani ufaulu umeongezeka.

Imeandikwa na Teddy Kilanga