Yanayochangia wasichana kujirahisisha kwa walimu

Wanafunzi wa kike wakisubiri usafiri jijini Dar es Salaam, wanafunzi wengi wamekuwa wakijichelewesha vituoni, huku wakidaiwa kuchagua mabasi ya kupanda. Picha na Sunday George

Wakati uzoefu ukionyesha walimu kuwanyanyasa kijinsia wanafunzi wao wa kike, imebainika katika baadhi ya nyakati wapo wasichana wanaowaweka walimu wao kwenye wakati mgumu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa malezi duni ya wanafunzi hao, ugumu wa maisha wanaopitia baadhi yao, yanawasukuma wasichana kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi sio tu na walimu wao, lakini hata watu wengineo wakiwamo makondakta.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kuna matukio kadhaa ya wanafunzi wa kike kuwataka kimapenzi walimu na watu wengineo, wakitumia njia ya kujirahisisha ili kukidhi mahitaji yao yakiwamo hata ya kimaisha.


Simulizi ya mwalimu Heri

Mmoja wa waathirika wa vitimbi vya wasichana shuleni ni mwalimu Bakari Heri aliyewahi kufanya kazi hiyo kabla ya kuacha katikati ya miaka ya 2000. Anasema aliwahi kukutana na vitimbi vya msichana mmoja, ambaye aligundua kuwa alikuwa akiishi na mzazi mmoja ambaye pengine hakuwa na msaada mkubwa wa kumwezesha mwanawe kujikimu akiwa shuleni. Lakini kubwa zaidi ni kile ambacho mwalimu huyo hakuweza kubaini kama wasichana waliomtaka walifanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha au tabia tu mbovu.

Anasimulia: ‘’Mimi nilihitimu ualimu katika chuo kikuu kimoja hapa nchini miaka ya mwanzoni mwa 2000. Nilibahatika kufundisha kwa miaka kama mitano hivi kabla sijaacha.

‘’Ni kweli kuna walimu ”viwembe” nami hilo nililiona nikiwa mwalimu, lakini pia niseme uhusiano wa mapenzi shuleni ni suala la pande mbili. Kuna walimu wanaowarubuni watoto, lakini pia wasichana wenyewe wapo wanaojirahisisha au kujitegesha kwa walimu. Na kuna sababu kama vile msichana kutaka msaada wa kimasomo au wa kifedha.

‘’Haya yote ndiyo yaliyonikuta mimi. Inaweza kuwashangaza wengi, lakini nikiwa mwalimu nilishatakiwa na wanafunzi watatu, wawili naweza kusema walizunguka kunitaka kimapenzi,lakini huyu wa tatu, niseme ilikuwa balaa. Alinikabili uso kwa uso na kunitamkia kuwa ananipenda na angetamani niwe naye maishani.

Nilikuwa nasikia kuwa mwanamume anaweza kutakiwa na mwanamke siku hiyo nilithibitisha kwani yule msichama ” alinibananisha” kwa hoja za kunitaka kiasi cha kumshangaa alipata wapi ujasiri ule. Hao wengine wawili ni habari nyingine, lakini kwa suala la tabia za wanafunzi wa kike kuwapa wakati mgumu walimu wao, mimi ni shuhuda na wala sioni uzito kusema wasichana nao ni tatizo.’’


Wasemavyo walimu

Mwalimu Japhet Thomas mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, anasema matukio ya wanafunzi wa sekondari kuwataka walimu kimapenzi yapo japo kwa kiwango kidogo tofauti na hali ilivyo vyuoni. Anasema matukio hayo hayahusishi wanafunzi kuhitaji kufaulu, wanasukumwa tu na hisia za ngono.

"Hasa kidato cha pili ndio nimeona wana matatizo haya, wachache pia wapo shule za msingi. Nakumbuka nimeripoti shule kuanza kazi baada ya muda, kuna mwanafunzi alinifuata akanieleza wazi kabisa kwamba ananitaka kimapenzi na alikwenda kuwatangazia wenzake,"anasema.

Licha ya kutotilia maanani alichoambiwa na mwanafunzi huyo, baada ya muda binti huyo aliyekuwa kidato cha pili alianza kujitapa kwa wanafunzi wenzake anatoka kimapenzi na Mwalimu Thomas hivyo wenzake wasimsogelee.

"Nilishangaa sana zile habari. Lakini pia kuna wanafunzi wa kike kama watatu walianza kugombana wakinitaka kimapenzi ila sikuwahi kuruhusu ujinga huo na niliwachukulia hatua kali na kuwaeleza lengo la wao kuwa shuleni kusoma tu,"anasema.

Kwa upande wake, mwalimu Jamali Jaffary wa Dar es Salaam anasema watoto wa Sekondari kuanzia miaka 15 hadi 20 wana mihemko ya kimapenzi.

"Unaweza ukawa unafundisha mwanafunzi anakurembulia huku shati kalegeza vifungo vya juu. Sasa haya ni majaribu lakini kwa sababu tumefundishwa maadili, nakemea tabia hiyo inapojitokeza na huyo mwanafunzi anaona hapa hapaingiliki,"anasema.


Ushuhuda wa wasichana

Japo yeye hakuwahi kumtega mwalimu, Theresia Paul, mwanafunzi jijini Dar es Salaam, anasema baadhi ya marafiki zake, hutamani kutembea na walimu ili wapate simu na kupata baadhi ya mahitaji.

"Kuna mwanafunzi mwenzetu yeye alikuwa anampenda mwalimu wetu wa hisabati tukiwa kidato cha tatu, ili aturingishie kwamba ana bwana na apate matunzo, ila alisimamishwa shule baada ya kupewa maelekezo ampeleke mzazi, adhabu ilipoisha akarudi shule akahamishwa,"anasema

Naye Zubeda James, anasema ameshuhudia namna wanafunzi wanavyojirahisisha kulala na wahadhiri wao chuoni ili waongezewa alama, lakini baada ya tukio hawapati walichokusudia.

“Mwanafunzi haingii darasani, kazi inatolewa hafanyi. Anaona njia ni kumfuata mwalimu sasa naye mwalimu ni binadamu na ana hisia. Anajua mwalimu ana udhaifu anakwenda mezani kwake kuongea naye huku kwa kiwango fulani matiti yanaonekana wazi…anaeleza.


Si shuleni hata vyuoni hali mbaya

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Bujo Ambosisye, anakumbuka namna akiwa mkuu wa idara chuoni hapo, kazi hiyo ilipokuwa mzigo mzito kwake.

Anasema baada ya kupata nafasi hiyo, wanafunzi wa kike walioanguka kimasomo, walikuwa wakimkabili na kutaka awasaidie huku wakisema wako tayari kumpatia chochote atakachohitaji.

“Mtu anakumbia nisaidie mwalimu nitakupa chochote, sasa najiuliza kwa hali ya kawaida binadamu hana vitu vyote, sasa hicho chochote ni nini”anasema.

Ambosisye anasema kauli za wanafunzi hao hakuziafiki, alizikemea vikali, kwani maadili yake ya kazi hayakuruhusu tabia hiyo.

Mhadhiri mwingine, Vicent Mpepo wa chuo hicho anasema changamoto ya wanafunzi kumlaghai kingono, amekuwa akikumbana nayo na hali hiyo inatokana na wanafunzi kutojisomea.

“Alikuja mwanafunzi analia ananiambia nitakupa unachotaka. Nilimjibu aache dharau hana cha kunipa,tangu nilipomwambia hivyo sikumuona tena, kwa hiyo haya matukio yapo na yanatuweka kwenye wakati mgumu sana,”anasema.


Uhusiano na makondakta

Kondakta wa gari basi linalofanya safari kati ya Simu2000 na Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Frank Brian anakiri kuwapo kwa baadhi ya wanafunzi wenye uhusiano na makondakta, huku akisema wasichana hao hujenga mazingira ya uhusiano huo ili wapate fedha.

"Unawakuta wamesimama vituoni wanaranda randa, wengine wanatutaka wakiamini pesa tunazoshika ni zetu na madereva wetu, kwa hiyo anajua akitembea na mimi, nitampa hela maana anaziona. Hisia tu ndio zinawapelekesha,"anasema Frank.

Anasema wapo baadhi ya wanafunzi huwadanganya makondakta kwa kujenga nao uhusiano na baadaye kuwaachia namba feki za simu na kushuka bila kulipa nauli.

Kwa upande wake, John Urio kondakta wa magari ya abiria ya Mnazi Mmoja hadi Gongolamboto, anasema uhusiano wa kimapenzi kati ya makondakta na wanafunzi, huchochewa zaidi na wanafunzi wenyewe.

"Mtoto anapanda kwenye daladala kazi yake ni kumtania kondakta tu, wakati mwingine anakuita alipokaa anakuambia ninunulie soda au akuulize una mpenzi, unajiuliza huyu anataka nini. Niseme ukweli kuna mwanafunzi moja mwaka jana alimaliza sekondari nilikuwa na uhusiano naye. Alikuwa ananipenda kweli lazima apande daladala yangu kila siku labda kwa siku ambazo sipo, anasema.



Kauli ya wazazi

Lucas Damian, mkazi wa Kinyerezi Dar es Salaam anasema ni muhimu wazazi kuwafundisha watoto maadili, ili kuwaepusha na uvunjifu wa maadili unaoweza kuwa na hatari.

“Ukiona mtoto anatumia rushwa ya ngono kupata kitu ujue msingi wa malezi yake una shida. Ni lazima mzazi kumjenga mtoto kwenye msingi wa kuwa na hofu ya Mungu,”anasema.

Naye Husna Kizinga mkazi wa Tabata anasema, tabia mbaya ya wanafunzi inachangiwa na wazazi ambao huacha kuwalea watoto wafikapo vyuoni, wakiamini kuwa wameshakua na wanaweza kujisamamia.

“Mtoto anapoingia chuo anaonekana tayari ameshakua. Hilo ni jambo la hatari unampa uhuru mkubwa mtoto ambaye ametoka kwenye ulinzi wa mzazi sasa anaongozwa na watu wasio na tabia njema, lazima afanye kinyume na maadili,”anasema.


Mtazamo kisaikolojia

Mhadhiri wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Christian Bwaya anasema mwanadamu ana mbinu nyingi kupata anachokitaka, hasa akijua mwenye nacho ana mamlaka.



Anasema upo wakati mtu anatumia mbinu za kuonewa huruma, mwingine anatumia uongo, rushwa, alimradi apate anachokitafuta.

“Wanafunzi kama binadamu wengine nao wana mbinu hasa wanapogundua wanaweza kupata upendeleo kwa mwalimu, ambaye ni mtu muhimu mwenye maamuzi yanayoamua hatima yake kitaaluma.Kuna wanaofikiri kuwa karibu na mwalimu, kumtendea wema, kunaweza kutengenezea mazingira ya kudaiwa arudishe shukrani kwa mlango wa nyuma,”anasema.

Bwaya anaeleza kuwa, ni lazima mwalimu mwenyewe afungue milango na kumwonesha mwanafunzi kuwa inawezekana.

Hata suala la rushwa ya ngono, Bwaya anasema rushwa ngono inategemea mambo mawili makubwa, ikiwamo namna mwalimu anavyojiweka.

Anasema kuna namna mwalimu akionyesha milango iko wazi na uwezekano huo wa uhusiano wa ngono upo, kweli watakuja.

‘’Ndio maana wapo walimu wengi tu vijana watanashati na bado hawafuatwi fuatwi na wanafunzi.Kimsingi inaanza na mwalimu mwenyewe. Ukijiweka kama mtu usiye na mipaka, unayefikika na wanafunzi, watakuja. Ukijiwekea mipaka, ukaisimamia, wanafunzi watakuheshimu na wataogopa kukufikia labda kama mtu ana changamoto kubwa na hana aibu,’’ anaeleza.

Anasema ingawa ni kweli wapo wanafunzi wanaoweza kutumia rushwa ya ngono kupata alama, bado mwenye nguvu ya kuamua anabaki kuwa mwalimu.