Zahanati mbili zasaidia wanawake 600 kujifungua kwa mwezi

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - Tamisemi, Dk Festo Dugange

Muktasari:

  • Zahanati hizo zipo katika mikoa ya Geita na Tabora ambazo hata hivyo zinatajwa kuwa majengo yake yamechoka na zinahitaji marekebisho.

Dodoma. Hivi ulijua kuwa hapa Tanzania kuna zahanati mbili ambazo zinasaidia wanawake 600 kujifungua kwa mwezi.

Zahanati hizo zenye idadi kubwa ya wanawake wanaojifungua ni ile ya Nkome wilayani Geita ambapo kwa mwezi wanawake 400 hujifungua, nyingine ni iliyopo Manispaa ya Tabora ijulikanayo kama Town klinik, amapo wanawake 200 hujifungua kila mwezi.

Idadi hiyo inafanya zahanati hizo mbili, kuzalisha wanawake 600 kwa mwezi, huku kukiwa na wanastani wa watoto 7,200 wanaozaliwa katika zahanati hizo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Sera ya Afya, Serikali inakusudia kila kujenga zahanati katika kila kijiji nchini, huku vituo vya afya vikijengwa katika kila kata.

Bunge limepokea taarifa hiyo leo Oktoba 31, 2023 wakati Naibu Waziri wan chi Ofisi ya Rais Tamisemo Dk Festo Dungande alipokuwa akijibu maswali ya wabunge katika kipindi cha maswali na majibu.

Katika kipindi hicho, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Munde Tambwe ameuliza ni lini Serikali itapanua na kuboresha ujenzi wa Zahanati ya Town Kliniki ya Tabora ambacho wanawake 200 wanajifungulia hapo kwa mwezi.

Wakati Mbunge huyo akiuliza swali hilo, wabunge wenzake walionekana kushangaa idadi hiyo, ndipo ilipofika zamu ya Mbunge wa Geita Vijiji Joseph Kasheku maarufu Msukuma ambaye aliuliza swali akiitaja Zahanati ya Nkome kuwa wanawake 400 wanajifungua hapo kwa mwezi, idadi iliyoonekana ni kubwa kwa zahanati.

“Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa katika Zahanati ya Nkome kuna wanawake 400 wanajifungua kwa mwezi, Serikali itaendelea kufanya maboresho na kuongeza majengo katika zahanati ikiwemo kupepeleka watumishi ili kuboresha huduma zinazotolewa hapo,” amesema Naibu Waziri Dk Dugange wakati akijibu swali hilo la nyongeza.

Awali katika swali namba mbili Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Minza Mjika ameuliza ni lini Serikali itajenga Zahanati katika Kata ya Binza katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ili kuwasaidia wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani kupata huduma.