Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zahanati yadaiwa kutelekezwa Shinyanga

Jengo la zahanati katika Kijiji cha Isela lililojengwa kwa nguvu za wananchi na serikali kutelekezwa tangu mwaka 2021 baada ya kukamilika.

Muktasari:

  • Jengo hilo la zahanati lililopo katika kijiji cha Isela Kata ya Samuye, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, lililojengwa kwa nguvu za wananchi na Serikali, limetelekezwa licha ya kukamilika tangu mwaka 2021.

Shinyanga.  Wakazi wa Kijiji cha Isela Kata ya Samuye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho iliyotelekezwa hali inayowalazimu kutembea zaidi ya kilomita nne kwenda kituo cha afya Samuye.

Wakizungumza leo Januari 20, 2025 kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, baadhi ya wananchi wamesema jengo hilo linaendelea kuchakaa kutokana na ujenzi wake kushindwa kukamilika zaidi ya miaka 10.

Saliboko Masunga mkazi wa Kijiji cha Isela amesema zahanati hiyo ilianza kujengwa tangu mwaka 2010 na kukamilika mwaka 2021, lakini hakuna huduma inayotolewa mpaka sasa huku jengo likianza kuchakaa.

“Katika kujenga jengo hili wananchi tumetumia nguvu kubwa ikiwemo kununua mabati 100 na fedha nyingine zilizotoka halmashauri, tunaumia sana tunaona nguvu zetu zinapotea bure bila kufikia lengo tulilokuwa tumekusudia,” amesema Masunga.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Isela, Monica Manyanyio amesema changamoto ya kukosa huduma za afya karibu inawalazimu kutembea zaidi ya kilomita nne kwenda makao makuu ya Kata Samuye kupata huduma.

Ameiomba Serikali kusikia kilio chao kwa kukamilisha ujenzi huo ili iweze kuanza kutoa huduma na kuwanusuru kinamama wajawazito wanaotembea umbali mrefu kwenda Samuye.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Dk Nuru Yunge amesema wanatarajia kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025 ambapo wametenga Sh25 milioni kumalizia sehemu iliyobaki.

Amesema zahanati hiyo bado kuna miundombinu ambayo haijakamilika vikiwemo vyoo na vichomea taka, ambapo mwaka 2023 halmashauri ilitoa Sh10 milioni kwenye ujenzi wa zahanati hiyo.

Kufuatia madai ya wananchi kukosa huduma za afya karibu, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ametoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri ya Shinyanga kabla ya Julai mwaka huu zahanati hiyo iwe imeshaanza kufanya kazi.

“Hakuna kusubiri mpaka fedha za Julai huku wananchi wanaendelea kutaabika haikubaliki tafuteni fedha mkamilishe ujenzi zahanati ianze kufanya kazi, wananchi wamepambana na Serikali imetoa fedha halafu bado jengo limetelekezwa,” amesema Mtatiro.