Zaidi ya nusu ya miamala ya fedha haipiti mifumo rasmi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha ameagiza taasisi za fedha kuongeza ubunifu

Dar es Salaam. Serikali imesema asilimia 60 ya miamala nchini haipiti kwenye mifumo rasmi, hivyo imezitaka benki na taasisi za fedha kuongeza ubunifu ili sekta hiyo ichochee maendeleo ya uchumi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hayo leo Alhamisi wakati wa uzinduzi wa mauzo ya hisa za Maendeleo Bank PLC. Amesema ni asilimia 40 tu ya miamala ya kifedha hupita katika mifumo rasmi.

Dk Mpango amesema sekta ya benki ni muhimu katika kukuza uchumi kupitia huduma za fedha kwa kutumia simu za mkononi.

Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza Afrika, kwa kusogeza karibu huduma za kibenki kwa wananchi.

Dk Mpango ameitaka Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA) kuongeza nguvu katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa umiliki wa hisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Maendeleo, Ibrahimu Mwangalaba amesema tangu ianzishwe mwaka 2013 imeongeza matawi hadi kufikia matatu.

Amesema mwaka 2015 benki ilipata faida ya Sh175 milioni na mwaka iliongezeka na kufikia Sh555 milioni.

Kwa kipindi cha miaka minne amesema benki imelipa kodi ya Sh2.42 bilioni.

“Leo tunashuhudia uzinduzi wa uuzaji wa hisa lengo likiwa kuongeza mtaji kwa Sh15 bilioni ambazo zitatumika kuimarisha shughuli za uendeshaji wa benki,” amesema.