Zimamoto kuajiri wafanyakazi 1,500

Muktasari:

Lengo ni kuongeza ufaAkizungumza leo Jumatano Agosti 29, 2018 katika wiki ya Jeshi la Zimamoto katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa, Lugola amesema ajira hizo zitaongeza kasi ya kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza maeneo mbalimbali nchini.nisi katika utendaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Dodoma. Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Serikali itaajiri wafanyakazi 1,500 kwa ajili ya jeshi hilo mwaka 2018/19.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 29, 2018 katika wiki ya Jeshi la Zimamoto katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa, Lugola amesema ajira hizo zitaongeza kasi ya kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza maeneo mbalimbali nchini.

“Tunatambua changamoto ya upungufu wa wafanyakazi katika kikosi hiki hivyo tutaajiri watumishi 1,500 ili kuongeza nguvu iliyopo,” amesema Lugola.

Waziri Lugola amevitaka vikosi vyote kuhakikisha vinafanya kazi kwa kujituma sambamba na kutoa huduma kwa jamii kulingana na mahitaji.

Katika hatua nyingine, Lugola amewaagiza wakurugenzi wote wa majiji pamoja na miji kutoruhusu ujenzi holela na badala yake wazingatie mipango miji.

“Tunatakiwa kuachana na ujenzi holela kwa sababu unasababisha vikosi vya zimamoto kushindwa kufika eneo la tukio kwa wakati,” amesema.

“Jambo hilo linawafanya waonekane hawafiki maeneo husika kumbe chanzo ni sisi wenyewe. Lazima tubadilike na viongozi wasimamie hili.”

Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, Thobias Andengenye amesema wanakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi ikilinganishwa na ukubwa wa nchi na idadi ya wananchi.

Amesema changamoto nyingine ni upungufu wa magari katika ofisi za mikoa na wilaya na kupendekeza magari 100 yatasaidia kufanya kazi kwa urahisi.