Zingatia haya unapompa mtoto maziwa mbadala

Saturday May 14 2022
Maziwa pcc
By Mariam Mbwana

Dar es Salaam. Maziwa ya mama ni chakula na kinywaji pekee kinachotosheleza mahitaji ya mtoto tangu anapozaliwa mpaka anapotimiza umri wa miezi 6.

Kutokana na umuhimu huo, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasisitiza watoto wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila kuongezewa kitu chochote kwa miezi sita ya mwanzo na baada ya hapo anaweza kuendelea kupewa maziwa ya mama pamoja na vyakula vyenye virutubisho hadi wanapofikisha miaka miwili au zaidi.

WHO inabainisha maziwa ya mama ni chanzo bora cha lishe kwa watoto baada ya kuzaliwa na hufanya kukua vizuri na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa.

Lakini kutokana na changamoto mbalimbali zinazosababisha mtoto kukosa maziwa ya mama, ikiwemo mama kufariki au kupata magonjwa yatakayochangia kushindwa kunyonyesha, husababisha maziwa mbadala hutumika.

Maziwa hayo ni pamoja yale ya fomula (maziwa ya kopo) na ya ng’ombe au mbuzi.

Wataalamu wanasema maziwa ya wanyama kama ng’ombe na mbuzi yana virutubisho vingi vinavyofaa kwa afya ya binadamu, lakini hawashauri maziwa hayo kupewa mtoto wa chini ya mwaka mmoja kwa kuwa yana kiwango kikubwa cha protini ambayo kwa umri wake huwa ni ngumu kumeng’enywa, hali inayoweza kusababisha mtoto kupata changamoto katika tumbo kama kutapika, kuharisha au kukosa choo.

Advertisement

Pia kwa mujibu wa tovuti ya healthchildren, maziwa hayo pia yana upungufu wa madini ya chuma, vitamin C na virutubisho vinginevyo ambavyo vinahitajika kwa ukuaji wa mtoto.

Maziwa pc

Mzazi aliyemnyweshwa mtoto wake maziwa ya ng’ombe alipokuwa na umri wa chini ya mwaka mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema katika kipindi hicho hakuwahi kuona mtoto wake akipata changamoto zozote za kiafya.

“Mwanangu alikataa kunyonya ziwa langu akiwa na umri wa miezi sita, nikashauriwa na daktari kumpatiwa maziwa ya ng’ombe lakini nilielekezwa namna ya kuyaandaa. Sikuwahi kushuhudia akipata changamoto iliyosababishwa na maziwa hayo,” anasema.

Naye Christina Daniel, mama wa watoto wawili, mkazi wa Kimara anasema mtoto wake wa mwisho akiwa na umri wa miezi saba alitokwa na vipele vyekundu na alipokwenda kwa daktari alielezwa mtoto ana mzio (allegy) na maziwa ya ng’ombe, hivyo aache kumpatia au kumchanganyia katika uji anaompa.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo anasema wazazi wanaowapa watoto wao maziwa ya ng’ombe bila ushauri wa wataalamu huweza kusababisha kupata upungufu wa madini chuma mwilini.

Anasema upungufu huo hutokana na maziwa hayo kuwa na kiasi kidogo cha madini chuma, hali inayosababisha mtoto kukabiliwa na upungufu wa damu mara kwa mara.

“Watoto wanaolishwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita bila chakula chochote kama inavyoshauriwa na wataalamu hupata madini chuma ya kutosha ambayo humkinga na kupata upungufu wa wekundu wa damu mpaka wanapofikia umri wa miezi sita na zaidi,” anasema.

Dk Gambo anasema maziwa yatokanayo na ng’ombe na mbuzi yana kiwango kikubwa cha protini kuliko kile kinachohitajika katika ukuaji wa mtoto wa binadamu kwa kuwa watoto wa wanyama hukua haraka, hivyo huhitaji protini nyingi.

“Hivyo ni vigumu kwa figo changa za mtoto wa binadamu kuondoa mabaki ya ziada ya protini mwilini yanayotokana na maziwa ya wanyama,” anasema.

Vilevile, daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Regency, Rahim Damji anasema maziwa ya ng’ombe huwa hayashauriwi kwa watoto wa chini ya mwaka mmoja kwa sababu ina kiwango kikubwa cha protini aina ya ‘casein’ ambayo huchukua asilimia 70, huku protini aina ya ‘whey’ ikichukua asilimia 30 ya protini.

Anasema aina hizi mbili za protini ni muhimu katika mwili wa mtoto, lakini ‘whey’ inahitajika kwa wingi kwani inasaidia mambo mengi, ikiwemo kurahisisha mmeng’enyo wa chakula, mtoto kupata choo vizuri na kumzuia kupata mzio kwa kiasi kikubwa.

Pia huzuia mtoto kupata changamoto mbalimbali, ikiwemo kuumwa na tumbo, kutokwa na vipele, kuharisha na kutapika. Dk Damji anasema kwa upande wa casein ambayo ipo kwa wingi katika maziwa ya ng’ombe au mbuzi hufanya mgando mzito usioyeyuka kwenye tumbo la mtoto, hivyo kusababisha mtoto kulia mara kwa mara, pia mmeng’enyo wa chakula kwenda taratibu.

“Hii ni moja kati ya sababu zinazofanya maziwa ya mama kushauriwa na wataalamu kutumiwa kwa mtoto wa chini ya mwaka mmoja, kwani yana kiwango kikubwa cha whey asilimia 60 na casein asilimia 40,” anasema.

Daktari huyo anasema maziwa ya mama ni bora kuliko yote kwa ajili ya ukuaji wa mtoto, lakini ikitokea changamoto inayofanya mtoto kukosa maziwa hayo, ikiwemo mama kufariki maziwa mbadala hutumika.

“Mbadala wa maziwa kwa mtoto inategemea uwezo wa familia, kama familia ina uwezo wa kumudu gharama za maziwa ya fomula (maziwa ya kopo) ambayo yanaweza kufanana angalau kwa baadhi ya virutubisho na maziwa ya mama japo haiwezi kuwa na virutubisho vyote kama kinga dhidi ya magonjwa ambayo hupatikana katika maziwa ya mama,” anasema.

“Inaposhindikana kupatikana fomula, maziwa ya ng’ombe yanaweza kutumika ila kwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ya namna gani ya kuyaandaa kwa ajili ya kumpatia mtoto,” anasema Dk Damji.

Anasema kitaalamu moja ya vitu vinavyoshauriwa kufanya kabla ya kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe ni kuyachanganya maziwa hayo na maji kwa vipimo kulingana na umri wa mtoto pamoja na kuzingatia usafi wa maji, maziwa na vyombo unavyovitumia katika kuchanganya maziwa hayo.

“Vipimo vinavyotakiwa katika uchanganyaji wa maziwa ya ng’ombe na maji hutegemea umri wa mtoto, inaweza kuwa kwa vipimo vinavyolingana au asilimia 75 maziwa na 25 yakawa maji.

“Kwa mfano kwa mtoto wa umri wa miezi mitatu vipimo huwa nusu kwa nusu, yaani kama maziwa safi yaliyochemshwa ni lita moja na maji safi yaliyochemshwa yanapaswa kuwa lita moja,” anaongeza.

Anasema kushindwa kuzingatia ushauri wa wataalamu juu ya namna gani ya kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe yanaweza kusababisha mtoto akapata changamoto za kiafya, ikiwemo kupata matatizo ya tumbo ambayo ni kuharisha, kutapika na hata kupata utapiamlo.

Anaongezea kuwa ni vema kwa watoto wanaotumia maziwa hayo pia kupatiwa na dawa za vitamini kwa kufuta ushauri wa daktari.

Advertisement