Zitto aahidi kuwasemea changamoto wananchi wa Kigoma

Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe akisalimia wananchi leo Jumamosi Machi 18, 2023 wakati akiwasili Uwanja wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Picha ba Erick Boniphace.

Muktasari:

  • Baada ya jana Ijumaa mvua kunyesha mjini Kasulu kuvunja  mkutano wa ACT- Wazalendo,  leo Zitto Kabwe amehutubia na kuwaeleza wananchi wa wilayani ataendelea kuwa sauti yao.

Kigoma. Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amewaambia wananchi wa Kasulu mkoani hapa kwamba ataendelea kuwa sauti zao bila katika kusemea changamoto zinazowakabili bila  kujali itakadi za vyama vya siasa.

Zitto ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 18, 2023 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni wilayani Kasulu.

"Nikija Kasulu nakuwa na furaha sana lakini jana (Ijumaa) mvua ilituzuia ila leo tunafanya mkutano. Watu wa Kasulu kwangu mimi ni nguzo, mlinipa nguvu miaka 10 iliyopita wakati nilipopata changamoto za kisiasa.

" Nawaahidi kuendelea kuwa sauti yenu pasipo kujali itakadi ya vyama vya siasa, kwa sababu kauli mbiu yetu ni Taifa la Wote, kwa Maslahi ya Wote mniamini sitowaangusha licha ya kutokuwa Bungeni," amesema Zitto.

Hata hivyo, Zitto amewaambia kuwa  binadamu ni watu wa kupita duniani na wakati wowote Mungu anaweza kumchukua, lakini watu Kasulu wanapaswa kukiimarisha chama hicho, kwa sababu ndio jukwaa sahihi la kusema changamoto zao.

"Lakini sisi binadamu tunapita ...wakati wowote Mungu anaweza kunichukua, lazima kutengeneza vyombo vitakavyosaidia kutetea watu, msichukulie poa kumuona Mwami (Zitto), kesho hayupo.

"Chukulieni  mfano  Zanzibar, kulikuwa na Maalim Seif (Sharif Hamad- aliyekuwa mwenyekiti wa ACT) leo hayupo lakini bado wapo imara, hii kwa sababu kuna mifumo imara aliyoiacha. Sasa ile habari ya kumpenda Mwami halafu kura mnakipa chama kingine sio sawa," amesema Zitto.

"Ili kuendeleza haya lazima muwe na jukwaa ambalo ni ACT- Wazalendo ili kukiimarisha chama, Kasulu ndio nguzo kubwa ya mabadiliko ya kisiasa mkoa wa Kigoma. Mabadiliko ya kisiasa ni muhimu katika kudai haki zetu, wembe ni ule ule wa miaka yote sasa tunaugeza upande wa pili," amesema.

Kutokana na hilo, Zitto amewataka wananchi wa Kasulu mapenzi yao kwake yahamie kwa ACT- Wazalendo. Amesema mtu akitaka kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo udiwani au uenyekiti wa vijiji na vitongoji aambiwe jukwaa sahihi ni ACT- Wazalendo.

Katika mkutano huo, Zitto aliwaahidi wananchi wa Kasulu kwamba atahakikisha changamoto katika mgogoro wa ardhi wa Kagerankanda ,akisema ameshaagiza wanasheria chama chake kusimamia suala hilo.

Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara, Dorothy Semu ameitaka Serikali kuongeza nguvu  katika kuboresha na kugharamia huduma za matibabu, akisema bado kuna malalamiko kwa wananchi hasa kwa wananchi wa hali ya chini.

"Afya imekuwa kama biashara yule mwenye uwezo anapata huduma bora, lakini asiyekuwa na uwezo inakuwa mtihani mkubwa kwake," amesema Semu.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema kauli ya chama hicho ya 'Taifa la Wote kwa Maslahi ya Wote' imelenga kila Mtanzania anufaike na rasilimali za Taifa, akimaanisha kila mwananchi apate huduma bora za matibabu.

"Tunataka miaka ijayo Tanzania iwe nchi yenye furaha kwa kila mwananchi awe mfanyabiashara, mwekezaji au mjasiriamali awe na amani na kutekekezaji majukumu yake pasipo bughuza," amesema Duni.