Zitto ashauri namna ya kumaliza sintofahamu ya wamachinga

Msajili, Zitto wavutana

Muktasari:

Kiongozi wa ACT-Wazalendo atoa ushauri na mikakati mbalimbali ya kumaliza sintofahamu ya wamachinga na Serikali, huku akisisitiza ubunifu utumike katika mchakato huo.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ubunifu zaidi unahitajika katika kumaliza suala la wamachinga ambao hivi sasa Serikali imeanza kuwahamisha kutoka maeneo yasiyoruhusiwa.

 Septemba 13 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu. Amesema licha ya Serikali kutoa fursa kufanya biashara kama njia ya ajira kwao, wamekuwa wakifanya kazi katika maeno tofauti na wakati mwingine kuziba maduka ya watu.

Mchakato huo umeanza kutekelezwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, ambako hivi sasa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanayotumiwa na wamachinga kufanya shughuli zao yamekuwa wazi baada ya kuondolewa kwa nyakati tofauti ambapo baadhi ya wamachinga wamekuwa wakilalamikia hatua hiyo.

Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Kigoma Kaskazini na Mjini kwa nyakati tofauti, ameeleza hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano yake na kituo kimoja cha redio kuhusu masuala mbalimbali ya siasa na mwenendo wa Serikali.


Katika maelezo yake Zitto, amesema suala la wamachinga linatokana na changamoto za shughuli za kiuchumi, akidai kuwa Taifa linazalisha vijana wengi kuliko uchumi wa kutengeneza ajira.

Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa sababu zinazosabisha vijana kuingia kwenye nguvu kazi, lakini hakuna ajira.

“Wanaamua kujiajiri wenyewe katika shughuli za umachinga, ni wajibu wa Serikali kutengeneza mazingira mazuri ili wafanyabishara kufanya shughuli zao bila bughuza.Nimesikia Kariakoo juzi watu wameondolewa na kuna malalamiko ya kwamba baadhi yao walikuwa wanapanga hadi kwenye njia za waenda kwa miguu.

“Ndio maana wanatakiwa kujenga mazuri ili wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwa ufanisi, nilipokuwa mbunge wa Kigoma kulikuwa na changamoto ya kina mama wa kata ya Mwanga kufanya biashara ya samaki barabarani nyakati za jioni. Lakini walikumbana na changamoto ya kufukuzwa,” amesema Zitto.

Amesema kutokana changamoto hiyo, baraza la madiwani la Kigoma Ujiji likatafuta suluhisho la kutenga mtaa mmoja unaofungwa kila siku kwa ajili ya kutoa fursa ya kina mama hao kufanya shughuli zaio kwa ufanisi ili kujiingizia kipato.

“Ni suala linalohitaji ubunifu zaidi badala ya kukimbizana na wamachinga, Serikali inatakiwa kukaa pamoja na wafanyabiashara hao sio viongozi wao pekee bali wenyewe ili kujadiliana nao na kuweka utaratibu bora wa kufanya shughuli zao,” amesema.

Katika mahojiano hayo, Zitto ameishauri Serikali masuala mbalimbali pia katika kumaliza sintofahamu ya wamachinga ikiwemo kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa kitakachowavutia vijana na kupunguza wimbi la watu kutoka vijijini kuhamia mjini kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo umachinga.

“Pia Serikali iimarishe viwanda vidogo vidogo ili kuleta ufanisi pamoja uwepo wa teknolojia itakayowavutia vijana wengi kukimbilia katika sekta hii,”amesema Zitto