Zuio la mikopo kwa halmashauri lamuibua Jafo, atoa wiki moja Ma DED kujisalimisha

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amezuia wakurugenzi watendaji wa halmashauri (DED) zote nchini kuacha mara moja kukopa fedha kwenye taasisi za fedha kwa madai ya kufanya miradi ya maendeleo.


Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi nchini Tanzania, Seleman Jafo ametoa wiki moja kwa wakurugenzi waliokopa fedha katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo wajisalimishe vingine hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo leo Alhamisi Novemba 28, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais wa Tanzania, John Magufuli kuzuia halmashauri kukopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Nawapa wiki moja walete taarifa ofisini ya kiasi gani walikopa na kwa matumizi gani, vinginevyo yatakayo kuja nyuma yake sitaki kusema hapa na wala hakuna kubembelezana sasa maana wanajua lakini wanafanya makusudi,” amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo ameagiza halmashauri ambazo zilishachukua fedha za mikopo ya miradi lakini hazijatumika kuzirudisha katika mabenki walikochukua mara moja ili kusudi wasiendelee kudaiwa.

Hata hivyo, Waziri Jafo ameshindwa kujibu kama riba watalipa kwa kutumia mfuko upi badala yake akasema kwanza apate taarifa.

"Kama wamekopa na hawajatumia fedha hizo zinapaswa kurudishwa mara moja na hakuna kuzitumia, lakini kama kiongozi alikopa na amehama halmashauri tutamsaka popote alipo ili atueleze, unajua wengi wanatengeneza riba kubwa kwa faida zao" amesema Jafo.

Ameitaja halmashauri ambayo imeshaingia mtegoni ni Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga ambayo ilikopa licha ya kuwa hakueleza kiasi huku Tamisemi ikizuia mkopo uliokuwa umeombwa na halmashauri ya Jiji la Arusha.

Amemuagiza Katibu Mkuu Tamisemi kuwakumbusha wakurugenzi kuhusu waraka wa Serikali uliotolewa Desemba 13, 2016 kuhusu kuzuia ukopaji kwa shughuli za maendeleo katika halmashauri hadi kwa maelekezo maalumu.

Jana Jumatano Novemba 27, 2019, Rais Magufuli akizungumza na wananchi wilayani Bukombe mkoani Geita alipiga marufuku wakurugenzi  watendaji wa halmashauri zote nchini kuacha  mara moja kukopa fedha kwenye taasisi za fedha kwa madai ya kufanya miradi ya maendeleo.

“Kama kuna mkurugenzi yeyote amekopa fedha azirudishe, mwenye mamlaka ya kukopa kwa niaba ya Serikali ni paymaster general wa Serikali ambaye ni Wizara ya Fedha pekee,” alisema Rais Magufuli