Zungu: Ipeni nafasi Serikali ifanye kazi

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu (kulia) akizungumza katika mahojiano maalumu na Mhariri wa Kanda ya Kati wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Nour Shija, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Naibu Spika, Mussa Hazzan Zungu amewataka Watanzania waungane na Serikali kwa kulipa kodi na kuacha tabia ya kutoomba risiti wanaponunua mahitaji.


Dodoma/Dar es Salaam. Naibu Spika, Mussa Hazzan Zungu amewataka Watanzania waungane na Serikali kwa kulipa kodi na kuacha tabia ya kutoomba risiti wanaponunua mahitaji.

Zungu alisema hayo juzi ofisini kwake bungeni alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu umuhimu wa kodi na vyanzo vyake.

“Wananchi tuungane na Serikali yetu awamu ya sita ya Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan), tulipe kodi, tuache tabia ya kwenda dukani na kutochukua risiti,” alisema Zungu.

Zungu ambaye ni Mbunge wa Ilala mkoani Dar es Salaam alisema “Mimi lazima nimpongeza mheshimiwa Rais (Rais Samia) pesa hizi zimefanya kazi kubwa sana, kwenye jimbo langu nimeshapata bilioni mbili za barabara. kituo cha afya cha milioni 700, pesa zingine za shule zaidi ya milioni 50 za kuboresha madarasa yetu. Na wananchi wajivunie,” alisema.

Alisema licha ya Serikali kusikia kilio cha wananchi waliokuwa wakiumia kutokanana tozo, pia ameitaka Serikali kuongeza wigo wa kodi hasa kwenye matumizi ya intaneti, lakini siyo kwa kutoza bando.


Mapato ya intranet

Zungu alisema Serikali inapoteza mapato mengi sana kwenye ‘internet gateway’ kwa kuwa inalazimika kulipia gharama hizo kwa watoa huduma hiyo walio nje ya nchi.

“Kuna nchi moja ya Afrika Magharibi ambayo inazalisha mafuta. Lakini, GDP (pato la ndani) yao ya mafuta haiwezi kushindana na GDP kwenye intarnet.

“Intarneti ndiko kwenye soko kubwa la dunia na hasa kwa vijana. Kwa hiyo, tuna gateway ambazo mashirika ya simu yanatumia kupitisha huu mtandao wa intarnet, lakini kuna gharama tunalipa nje ya nchi, lazima tulipe hizi gharama, sasa kwa nini Tanzania tusiwe na gateway ya kuwa na umiliki wetu, tumiliki wenyewe.

“Tukimiliki wenyewe hata makampuni yatakuja kupata huduma kwenye taasisi ya Serikali, badala ya kulipa hizi pesa nje ya nchi zitabaki ndani.

“Kwa hili kuna biashara kubwa sana, lakini hili nitapigwa vita, watu wengi wanapenda kujilimbikizia mali wao wenyewe, hawataki umma wapate pesa na hii tukifanya tutakuwa na sehemu moja ya huduma za intanet.

“Tutasaidia vijana kuwa watoa huduma za intarnet, wawe na ‘internet café’ zao, kwa mafunzo watakayopewa kutoka chuo maalumu ambacho mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ameahidi kukitengeneza na wataweza kuwa watoa huduma kama zinavyofanya nchi nyingine wajipatie mapato makubwa wao na Serikali,” alisema Zungu.

Alitoa mfano wa watumiaji wa intaneti Tanzania kwamba wako asilimia 25 wakati nchini Kenya wako asilimia 43.

“Tuko takribani watu milioni 60, watumiaji wa intaneti ni asiimia 25 ni sawa na watu kama 15 milioni ni ndogo. Kwa hiyo inaonyesha vijana hawachangamki kuwa na simu janja na kwa mkakati huu ambao tunakwenda nao karibu wote wenye simu watakuwa ni watoa huduma, ili na wao wajipatie kipato kizuri,” alisema Zungu.


Wanaotukana mtandaoni

Akizungumzia wanaotoa mashambulizi dhidi Serikali au watu kwenye mitandao ya kijamii, alisema wanaofanya hivyo wajue kila ujumbe wanaotuma wanalipa kodi.

“Kikubwa ili kuepukana na ugomvi huu kuwe na walipaji kodi wengi. Tanzania tuko watu milioni 60, lakini walipaji wa kodi hawafiki milioni sita,” alisema.


Mapato ya nchi

Pia, Zungu alitoa angalizo kuhusu mapato ya nchi yanavyopotea kutokana na mfumo wa ukusanyaji mapato kutoingiliana.

“Kwa mfano, bandarini utakuta mfumo wa kodi hauendani sawa sawa na mifumo inavyotakiwa iwepo. Kwa hiyo kuna mfumo wa Hi-Tech ambao zote zinatakiwa kuwa ‘integrated’ (jumuishi) ili kuwezesha usomaji wa mapato ya Serikali na mtu mmoja au eneo moja,” alisema.

Alifafanua “Kwa mfano bandari ya Dar es Salaam inakusanya Sh95 bilioni kwa mwezi, wakati kuna bandari nchi jirani inakusanya Sh333 bilioni kwa mwezi.

“Hii hoja yangu ya kwanza kwa Serikali, tuna udhaifu katika ukusanyaji mapato.

“Hoja nyingine kwa Serikali ya namna inavyopoteza mapato, waangalie tozo na miamala kwa watoa huduma wa mabenki na kampuni za simu. Hawa nao wapunguze kwa kuwa Serikali imepunguza tozo zake.

“Utakuta sasa hivi gharama za ‘levy’ za benki zinatofautiana katika benki na benki, nyingine zinachaji ‘levy’ kubwa zaidi ya hata ile inayochukua Serikali.

“Serikali inapata Sh4,000 benki inapata Sh13,000 kwa muamala mmoja, lakini watu hawaoni hiyo, hoja ni kuwe na udhibiti au hawa watu wahojiwe, zitazamwe, zipitiwe upya kama zina uhalali, labda wanasema wana gharama za mishahara, uendeshaji benki zao, lakini zipunguze yale makali kwa watu, zisiwe kwa kiwango kikubwa sana.

“Kwa hiyo niiombe Serikali walitazame hili upya wajiridhishe hizi tozo kweli ni halali na zinastahili. Wakae na benki wazipunguze na kuwapunguzia mzigo wananchi, kama ilivyofanya Serikali kwenye tozo zao.

“Kile kidogo inachopata Serikali inakipeleka kwenye maendeleo, lakini mabenki na kampuni za simu zinachukua pesa nyingi sana. Sasa hilo wakalitizame ndio ilikuwa hoja yangu,” alisema Zungu.


Tozo za Serikali

Alisema pamoja na Serikali kuondoa tozo bado malalamiko yapo, hivyo aliwaomba wananchi waiache Serikali ifanye kazi, kwa kuwa wameunda kamati inayoshirikiana na Bunge kufanyia kazi suala hilo.

“Masuala ya tozo yako serikalini na imeshapunguza baadhi ya maeneo, bado yako malalamiko na inayatazama, tuache Serikali wafanye kazi,” alisema.