Mazoezi yanayoboresha tendo la ndoa haya hapa

Mwanasayansi wa tiba bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk Anold Kegel wa Marekani ni mgunduzi wa mazoezi yajulikanayo Kegel yenye kuboresha tendo la ndoa kwa wanawake.

Uzoefu mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kiafya kwa wanawake kulimwezesha kubaini udhaifu wa misuli ya kitako cha kiuno kwa wanawake waliotoka kujifungua. Wazo lake hilo ndiyo lilimfanya kugundua mazoezi hayo yanayochangia kuboresha afya ya uzazi kwa upande wa tendo la ndoa, ingawa kiujumla mazoezi mepesi yote yana mchango mkubwa kwa binadamu katika afya ya uzazi.

Kwa Dk Kegel alilenga mazoezi yanayoimarisha misuli ya kiunoni, ndiyo yanayoboresha tendo la ndoa hatimaye kufanyika kwa ufanisi. Pia alikuja na kifaa na mazoezi yanayosaida kukabiliana na tatizo la kushindwa kuzuia mkojo.

Na hii ndiyo sababu kubwa mazoezi haya yakaitwa mazoezi ya Kegel ambayo tafiti za kitabibu yanayathibitisha kusaidia kuimarika kwa tendo la ndoa kwa wanawake. Sababu ni kutokana na mazoezi haya kusaidia kuimarisha nguvu ya misuli muhimu ya kitako cha kiuno ambayo ina athari chanya katika kufanyika kwa tendo hilo kutokana na matukio yanayomkuta mwanamke ikiwamo wakati wa kujifungua, upasuaji, ajali za kiuno, umri mkubwa, shambulizi la magonjwa na unene huweza kudhoofisha misuli.

Misuli hii iko katika kiuno ndani ambayo huipa egemeo ili kushikilia nyumba ya uzazi, kibofu cha mkojo, uke na eneo la mwisho la mfumo wa chakula.

Kuimarika kwa misuli ya eneo hili na kuwa na nguvu husaidia kuongeza msisimko wa kilele cha mapenzi kwa wenza wote wawili, kwani misuli hiyo huikandamiza na kuibana misuli ya uke kwa ufanisi.

Pia ni vizuri kwa ujumla kufanya mazoezi yale mapesi ikiwamo kutembea, kukimbia kasi ya wastani, kuogolea, kucheza muziki, kuendesha baiskeli, kuruka kamba na mazoezi mchanganyiko ya gym, ili kuboresha afya ya mwili.

Mazoezi kama haya yanasaidia kuboresha kiwango cha vichochezi vya uzazi, hivyo kuboresha afya ya uzazi ikiwamo kumsaidia mwanamke kuwa na mzunguko usioyumba.

Kwa kawaida mazoezi ya Kegel huitajika kufanyika wakati kibofu cha mkojo kikiwa kitupu huku ukiwa umelala chali chini eneo ambalo lina ugumu wa wastani, ili kukufanya usione karaha.

Unaweza kuchagua eneo lolote ambalo kwako itakua ni burudani kulifanya ikiwamo nyumbani, ofisini na hata katika vyombo vya usafiri. Zoezi hili huweza kulifanya bila mtu mwingine kubaini unachokifanya.

Zoezi hili hufanyika kwa kuikaza misuli ya kitako cha kiuno na ushikilie hivyo kwa muda wa sekunde 3 hadi 5.

Baada ya muda huo kupita acha kuikaza na tulia ili kuilegeza. Rudia kufanya hivyo mara 10 na ufanya mzungo huo mara tatu kwa siku au kila baada ya saa nane yaani asubuhi, machana na jioni. Unaweza kuijua misuli hii pale unapokuwa umebanwa na haja ndogo kali na huku ukiwa unaizuia isitoka kwa kubana haja hiyo isitoke. Misuli inayokuwezesha kufanya hivyo ndiyo hiyo iliyozungumzwa na Kegel.

Ubanaji wa misuli hiyo usiendane na ubanaji wa misuli mengine iliyo jirani ikiwamo ya tumboni, mapajani na makalioni na upumuaji wake hutakiwa kuendelea kama unavyofanya mazoezi mepesi.

Mazoezi haya kama ilivyo mengine ili kupata matokeo makubwa hutakiwa kuyafanya mara kwa mara kwa kufanya katika siku tano za wiki. Ukiacha faida ya kuibana misuli ya uke kwa ufanisia, pia zoezi hili huwa na faida ya kusaidia kuimarisha uke hivyo ni faida wakati wa kujifungua.

Kwa anayependa kuongeza ufahamu zaidi anaweza kununua vitabu vya Kegel au kupakua apps katika simu janja au video zenye kuelekeza mazoezi haya.