Uhusiano wa kukaa muda kwa mrefu na maumivu ya mgongo

Muktasari:

Unapokaa kwenye kiti kwa zaidi ya nusu saa hadi saa tatu bila kusimama, unakuwa hatarini kupata ugonjwa wa Chronic back pain unaohusisha maumivu kwenye uti wa mgongo.

Huenda ukawa ni miongoni mwa watu wengi waokaa kwenye viti kwa muda mrefu bila kufanya shughuli nyingine inayo sababisha mtu kutembea .

Unapokaa kwenye kiti kwa zaidi ya nusu saa hadi saa tatu bila kusimama, unakuwa hatarini kupata ugonjwa wa Chronic back pain unaohusisha maumivu kwenye uti wa mgongo.

Maumivu ya mgongo ni mfano wa homa inayobeba aina mbalimbali za maradhi kupitia sababu za kimazingira, aina ya maisha maumbile.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya uti wa mgongo wa binadamu una pingili 33.

Katikati ya pingili moja na nyingine kuna kipande cha diski kinachosaidia pingili zisisagane.

Kila unapoinama, kukaa au kuchuchumaa kwa muda mrefu husababisha mgandamizo mkali hivyo kuhatarisha uimara wa diski.

Mtaalamu wa mifupa, kutoka Kitengo cha upasuaji wa mgongo na mishipa ya fahamu katika Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Lemeri Mchome anasema maumivu ya mgongo huanza kidogo kidogo.

Anasema kwa wakati huo, tiba yake ni mazoezi ya mara kwa mara au kulala ili kunyoosha pingili za mgongo huo na maumivu hupotea.

“Kama ukiendelea kupuuza maumivu yanayoendelea kujitokeza kwenye mgongo inaweza kusababisha disk kucheza mahali pake au kusagika, hivyo inabidi ufanyiwe upasuaji,” anasema Dk Mchome.

Shuhuda azungumza

Hawra Shamte ni mmoja kati ya waliofanyiwa upasuaji Septemba mwaka 2013 katika Hospital ya Shalby iliyopo mji wa Ahmedabad nchini India.

“Nilipofika madaktari walinieleza chanzo ni kazi yangu iliyosababisha kukaa muda mrefu, umri na uzito wangu,”anasema mwandishi huyo mkongwe nchini.

Hawra aliyetibiwa kwa mwezi mmoja nchini India anadai kufanyiwa upasuaji na kuwekewa plastiki baada ya pingili zake kusinyaa na kuanza kugusana, zinazopatikana chini kiuno.

“Wanaziita Lumbar 5, Lumbar 4 na Lumbar 3, ikabidi wazitoe na kuwekewa plastiki zisizoyeyuka,” anasema Hawra.

“Nilitibiwa mwezi mmoja na baada ya miezi mitatu nilianza kutembea vizuri. Lakini kwa sasa siwezi kutembea umbali mrefu. Lakini madaktari walishangaa wagonjwa wengi sana kutoka Afrika Mashariki. Maumivu yake ni makali sana na gharama zake ni kama Sh17milioni, lakini siku hizo wanatibu nchini.”

Hawra ambaye kwa sasa ni mshauri wa huduma za habari anasema njia zinazosaidia kuepuka hatari ya kushambuliwa na ugonjwa huo ni pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara unapohisi maumivu na kuzingatia vyakula.

Anataja baadhi ya vyakula muhimu ni pamoja na bamia, kabeji na kuepuka nyama.

“Wakati naumwa niliweza kupunguza uzito kwa sababu ya chakula nilichokuwa napewa, vyakula ilikuwa ni bamia, bilinganya, mtindi na wali kidogo sana, daktari akikukuta unakula kuku anakasirika, ningekuwa ninazingatia mlo ule hadi sasa nadhani tatizo la uti wa mgongo ningekuwa nimesahau kabisa,” anasema Hawra.

“Lakini sasa si unajua chakula chetu Waafrika, tunafikiria Starchy (wanga) sana kuliko protini na vitamini, vyakula vingi ni tiba Afrika lakini hatuzingatii, tunataka kushibisha matumbo badala ya kuweka virutubisha katika mwili.”

Mtaalamu wa afya anasemaje?

Akizungumzia gharama za tiba, Dk Mchome anasema: “Hapa Moi tiba inaweza kugharimu Sh200,000 hadi Sh300,000 bila gharama za vipimo.”

Anasema uzoefu unanyesha watu saba kati ya 10 wanaofika kliniki hapo wanalalamika maumivu ya mgongo bila kujua chanzo chake.

Dk Mchome anasema kitalaamu dakika za kukaa zinategemeana na uzito, umri na afya ya mtu huku makadirio yakiwa ni kati ya dakika 45 hadi saa nne.

“Watu kati ya 20 hadi 30 tunaowapokea kliniki malalamiko yao yanafanana, atakwambia naumwa mgongo, mwingine ukiangalia diski kweli zimetoka anatakiwa kufanyiwa upasuaji lakini wengine unakuta misuli imekaza na inauma,” anasema Dk Mchome.

Hata hivyo, ukaaji ni sehemu tu ya chanzo kinachoweza kuathiri pingili zinazoanzia shingoni hadi chini ya makalio kwa kuwa kundi lingine lililopo hatarini ni wabeba mizigo, wanaobeba mikoba, kompyuta, mabegi ya shule na washindiliaji wa kutumia mashineza kutetemesha (Drillers).

“Sasa kuna namna ya ukaaji na kuna viti ambavyo haviruhusiwi kukaa sana kwa mfano viti vya chini sana vinavyoweza kusababisha mgandamizo wa diski hizo, sina hakika sana kama viti vyote vinavyotengezwa vinazingatia mahitaji hayo ya usalama wa mgongo,”anasema Dk Mchome.

Utengeneza wa viti

Ernest Fusi, fundi wa samani za ndani anasema huangalia masilahi ya kibiashara kwa wateja wasiojali ushauri wake.

Fusi ambaye amenza kazi hiyo mwaka 2001 wilayani Mbinga Mkoa wa Songea anasema kuna mitindo mingi ya viti vya kisasa isiyozingatia mahitaji ya kulinda uti wa mgongo.

“Kuna mteja anaweza kuja na picha ya viti vya kisasa lakini ukimshauri kwamba hivi vitakuletea shida ya mgongo anakuwa mbishi, ninaamua kumtengenezea kama anavyotaka kwa sababu niko kibiashara, lakini wako wanaokubaliana na ushauri wangu,”anasema Fusi.

Akitoa mfano, anasema kwa sasa anatengeneza viti kwa ajili ya matumizi ya wateja.

Fusi anasema viti vyote vinatakiwa kuwa na urefu unaomsaidia mkaaji asiiname na asikunje sana miguu.

“Mmiliki wa hiyo baa alitaka nimtengenezee viti vinne vya kisasa lakini nilipoangalia picha nikamshauri kubadilisha kidogo akakubali, picha zinaonyesha mtu akikaa anashuka sana kwa kujikunja miguu lakini nikamshauri kuvipandisha kidogo akakubali,”anasema Fusi akishauri wateja kuzingatia ushauri.

Katika biashara ndogondogo, kumbi za starehe na maeneo ya maofisini hali ikionyesha hatari zaidi kwa viti vinavyotumiwa na baadhi ya wahusika.

Abdulfatah Lyeme mwenye uzito zaidi ya kilo 90 anasema huzingatia ununuzi ya viti nyumbani kwake na kila mwaka hubadilisha magodoro kwa ajili ya kuzingatia mahitaji ya usalama wa mgongo.

Anasema ofisini ameweka utaratibu wa kusimama ofisini kila baada ya saa moja.

“Nyumbani siwezi nakuwa nimepumzika. Lakini wengi sana hawazingatii kazini. Mimi ninafahamu kwa sababu nimesoma vipimo hivyo kwenye kozi yangu ya uhandisi wa mitambo, tunaita chair ergonomic kwa maana ya kuangalia tabia za ukaaji, aina ya viti na godoro,” anasema.

Lyeme anashauri Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) kufanya ukaguzi wa kina kuhusu viti vinavyotumika ofisini na kuweka miongozo kwa waajiri na wasambaji wa samani hizo ofisini.